RAIS SAMIA AZINDUA KITUO CHA POLISI WILAYA YA IKUNGI, MKALAMA. AWATAKA WANANCHI KUTOJICHUKULIA SHERIA MKONONI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa vituo vya Polisi cha Wilaya ya Ikungi na Mkalama katika hafla iliyofanyika Oktoba 15, 2023.Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Kamillius Wambura, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
.........................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua
rasmi Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ikungi na cha Wilaya ya Mkalama mkoani
Singida na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha mara vitendo vya
kujichukulia sheria mkononi.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi
mkoani hapa aliyoianza Oktoba 15, 2023
alipokuwa akifungua kituo hicho cha
polisi alisema ujenzi wake umefanyika kwa thamani halisi ya fedha zilizotolewa
na Serikali.
" Nimeambiwa humo ndani mna
mambo mazuri mheshiwa IGP sina maswali kwenye thamani halisi ya gharama
za ujenzi wa kituo hiki kwa kweli sina maswali nakupongeza, nawapongeza wabunge
na jeshi la polisi kwa kazi nzuri na kupata jengo hili," alisema Rais
Samia.
Rais Samia aliwaambia wananchi hapo
ni makao makuu ya Polisi Wilaya ya Ikungi na ndani ya kituo hicho
imejengwa miundombinu mizuri sana kwa ajili yao.
"Kwa wale wahalifu hapa patakuwa ni nyumbani kwao lakini yale mambo ya
kuchukua sheria mkononi kwa sababu sasa jeshi la polisi lipo hapa sasa yaishe Serikali imejenga jengo zuri
huduma itatolewa humo kwa hiyo wananchi hakuna sheria mkononi mambo yote
yaletwe hapa yatashughulikiwa nisisikie tena watu wamechomana mishale,"
aliongeza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia aliwageukia watumishi wa jeshi la polisi na kuwaambia
kuwa na jengo zuri ni jambo moja na la pili ni kuwa na huduma bora kwa
wananchi.
" Unajua ukipata jengo zuri nimeambiwa mnanyumba za watumishi na
wakubwa huko nyuma ni mahali pazuri na
mnakaa vizuri na kupata moyo wa kufanya kazi nawaombeni muwatumikie wananchi
kwa kuwapatia huduma nzuri," alisema Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkadiriaji Majengo wa Jeshi la Polisi Mkaguzi wa Polisi, Asha Tuwa ujenzi
wa jengo hilo umezingatia miundombinu ya makundi mbalimbali ya watu wakiwamo
wenye ulemavu na kuwa ujenzi wa vituo hivyo umegharimu Sh. Bilioni 2.
Rais Dkt. Samia baada ya kufungua kituo hicho alipata fursa ya kuzungumza
na wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi eneo la Puma na kuwaomba kesho Oktoba
16, 2023 wafike Viwanja vya Bombadia ambapo kutakuwa na mkutano mkubwa wa
hadhara na kuzungumzia mambo mbalimbali.
Akitoa salamu kwa Rais Samia kwa niaba ya wanananchi Mbunge wa jimbo hilo,
Elibariki Kingu alimshuru Rais kwa kazi kubwa aliowafanyika ya kuwapelekea
miradi mingi ya maendeleo na ombi lake kubwa aliomba apewe Halmashauri ili iwe
rahisi kuwatumikia wananchi kutokana na ukubwa wa jimbo hilo.
Post a Comment