Header Ads

test

KICHWA CGA SONGEA KUREJESHWA NCHINI BAADA YA MWAKA MMOJA

 

Wizara ya Maliasili na Utalii imeunda Kamati ya Kitaifa inayosimamia urejeshwaji wa malikale zilizo nje ya nchi,likiwemo fuvu la Jemedari wa Wangoni Nduna Songea Mbano ambalo limehifadhiwa nchini Ujerumani.

Jemedari wa wangoni Songea Mbano na wenzake mashujaa wa vita ya majimaji 66 walinyongwa  nawajerumani mwaka 1906,ambapo wajerumani walikata kichwa cha Songea na kukipeleka nchini Ujerumani ambako kimehifadhiwa hadi sasa.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt.Emanuel Bwasiri akizungumza kwenye tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji mjini Songea,amesema Kamati ya kitaifa inaendelea vizuri kushughulikia suala hilo ili kuhakikisha malikale zote zilizo nje zinarejeshwa nchini.

“Sisi kama Wizara tunaamini mipango yote iliyowekwa ikienda vizuri,tunatarajia baada ya mwaka mmoja au miwili fuvu la Songea Mbano linaweza kurudishwa hapa nchini’’,alisisitiza. 

Hata hivyo amesema fuvu la Songea Mbano litakaporudishwa mawasiliano yatafanyika kati ya wenye  fuvu na serikali kuangalia namna fuvu hilo litakavyohifadhiwa hapa nchini.

Akizungumza kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi la mashujaa wa vita ya Majimaji,mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Mary Masanja ameiagiza Kamati ya Kitaifa inayoshughulikia urejeshwaji wa malikale zilizopo nje ya nchi likiwemo fuvu la Songea,kuhakikisha
wanatekeleza na kukamilisha kazi hiyo kwa haraka.

Amesisitiza kuwa serikali imedhamiria malikale hizo likiwemo fuvu la Songea Mbano zinarejeshwa hapa nchini na kuzifanya kuwa kumbukizi .

“Naomba kutoa taarifa rasmi kuwa miongoni mwa malikale zilizoshughulikiwa na kuhakikisha zinarejeshwa nchini ni Pamoja na fuvu la Songea Mbano ambaye ni miongoni mashujaa 67 wa vita ya Majimaji waliouwa kwa kunyongwa na wajerumani mwaka 1906’’,alisisitiza.


Amesema kumbukumbu za mashujaa wa vita ya majimaji zinawezesha kizazi cha sasa na kijacho kujifunza namna watanzania walivyojitolea maisha yao katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni.
Naibu Waziri Masanja pia amekemea vitendo viovu vinavyoendelea kujitokeza katika jamii vinavyoharibu mila,utamaduni na desturi za mtanzania ambapo amewaasa wazazi na walezi kusimamia maadili mema
kwa vijana wao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akitoa salamu za Mkoa kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi la mashujaa wa Majimaji, amelitaja lengo la tamasha hilo kuwa ni kuwambuka mashujaa 67 waliouawa kikatili na wajerumani kwa kunyongwa Februari
27,1906 ambao walizikwa katika eneo ambalo yamejengwa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.

Amesisitiza kuwa tamasha hilo linasaidia kukuza utalii wa utamaduni na  kurithisha mila na desturi zamtanzania kupitia matamasha ya utamaduni. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga amesema Makumbusho ya Taifa katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inalenga kuifanya jamii kuona umuhimu wa tamasha la Majimaji kwao na kuifanya ishiriki kikamilifu kutangaza
mila,utamaduni na desturi zao.

Ameyataja malengo ya tamasha hilo kuwa ni kutambua mchango wa historia ya mapambano ya wananchi dhidi ya ukoloni na kuwaenzi wapiganaji wa vita ya majimaji,kutoa fursa kwa wadau kutembelea na
kuona vivutio vya utalii vilivyopo kusini mwa Tanzania hususan mkoani Ruvuma na kuweka mkakati wa kuviendeleza.

Kaulimbiu ya tamasha la kumbukizi la mashujaa wa vita ya majimaji mwaka huu ni makumbusho yetu,urithi wetu kwa maendeleo ya utalii na uchumi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja akiweka silaha za jadi kwenye sanamu ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kwenye kilele cha kumbukizi ya mashujaa wa vita ya majimaji mjini Songea
Jemedari wa wangoni Nduna Songea Mbano aliyenyongwa na wajerumani yeye pamoja na mashujaa 66 wa vita ya majimaji Februari 27,1906 ,Hata hivyo wajerumani walikata kichwa cha Songea na kukipeleka nchini Ujerumani ambako kimehifadhiwa hadi sasa,serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kurejesha nchini fuvu la kichwa cha Songea Mbano pamoja na malikale nyingine zilizopo nje.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja akiweka shada la maua kwenye kaburi la pamoja ambalo wallizikwa mashujaa 66 wa vita ya majimaji ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji kwenye kilele cha kumbukizi ya mashujaa wa vita ya majimaji
Mgeni rasmi kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi la mashujaa wa vita ya majimaji Naibu Waiziri wa Maliasili na utalii mheshimiwa Mary Masanja akiwaongoza wananchi wa Manispaa ya Songea kwenye maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea
Chifu wa Tano wa Kabila la wangoni Nkosi Emanuel Zulu Gama akiwa shada la maua kwenye kaburi ;la pamoja la mashujaa wa vita ya majimaji Chifu wa Tano wa Kabila la Wangoni Nkosi Imanuel Zulu Gama baada ya kuweka zana za vita za jadi zilizotumiwa na mashujaa wa vita ya majimaji ndani ya makumbusho ya Taifa ya majimaji mjini Songea kwenye kilele cha tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya majimaji

No comments