Header Ads

test

BIOTEKNOLOJIA NI NYENZO MUHIMU KATIKA KUJIBU CHANGAMOTO KATIKA SEKTA MBALIMBALI.

Na: Calvin Edward Gwabara – Dar es Salaam. 
  
Imeelezwa kuwa mbinu ya matumizi ya Biotenlojia ya kisasa inaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kusaidia kupata majibu ya changamoto za sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Afya, Mazingira na nyingine za kiuchumi Barani Afrika na Duniani.
Hayo yamesisitizwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania na Mlezi wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST) Mhe. Adam Kigoma Malima wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu wanatoa taarifa za upotoshaji zisizo sahihi kuhusu teknolojia hiyo katika maendeleo ya watu na nchi lakini wamekuwa sehemu ya watumiaji wa mazao yaliyozalishwa kwa mbinu hizo kwenye sekta ya afya hasa Insulin na dawa zingine.

Mhe. Malima amesema watu hao wasio na nia njema na matumizi ya sayansi wamekuwa wakitumia nafasi ya uelewa mdogo wa watu kuhusu teknolojia hiyo nzuri kwa kupotosha na kutumia mifano inayotisha ili jamii na watu sera waogope na kuzuia maendeleo ya teknolojia kwa maslhi yao binafsi.

“Mimi binafsi kwa kushirikiana na viongozi wa BST na wadau wengine wenye uelewa wa kina kuhusu teknolojia hiyo tumewaita kwenye mikutano mbele ya viongozi wenye dhamana ya kufanya maamuzi ili kila mmoja wetu ajenge hoja na kutoa ushahidi lakini hakuna hata siku moja waliyotokea na hii ni Dhahiri kuwa wanatunga maneno na hawana ushahidi kuthibitisha kauli zao na hivyo kuwanyima nafasi Watanzania kunufaika na teknolojia nzuri kwa kuwaacha wakiteswa na wadudu,magonjwa na mabadiliko ya tabia nchi kila mwaka” aliffanua Mhe. Malima.

 Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan ni sikivu na inahimiza pia matumizi ya sayansi teknolojia na ubunifu katika kuleta maendeleo ya kichumi kama ambavyo ilikuwa wakati wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete iliyoanzisha tefiti za Bioteknolojia na kuweka miongozo na miundombinu na fedha zaidi ya Bilioni 20 Tanzania kuanza tafiti hizo.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wanasayansi kutokaa kimya pale wanapoona makundi hayo ya watu wasio na nia njema na Sayansi wanapotoa kauli za kupotosha umma na Serikali badala yake wasimame na kuweka ushahidi ili kuiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi ambayo yateleta tija kwa taifa kwakuwa baadhi ya wafanya maamuzi pia sio sio wote ni wataalamu wa teknolojia hiyo.

“Changamoto ya mvutano na upotoshaji kwenye matumizi ya mazao ya bioteknolojia upo dunia nzima na nchi mbalimbali zinatumia kwa wingi lakini upinzani huu unaonekana hasa kwenye kilimo kwa asilimia 85% lakini ni mdogo sana kwa asilimia 5% katika sekta ya afya sasa tunajiuliza tunawezaje kuacha wakulima wetu washindwe kupata mbegu zenye ukiznani dhidi ya magonjwa na wadudu na mabadiliko ya tabia nchi wakati ufumbuzi upo.” alieleza Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa kuanzisha kozi ya Bioteknolojia kwenye vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo,Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu ch Dodoma, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na vingne ili kuongeza wataalamu katika fani hiyo na kuomba nchi iwatumie kusaidia Taifa.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Peter Msolla amesema BST inapongeza jitihada za Serikali kwa kuznisha program ya Building better tomorrow (BBT) ambayo inalenga kuwafanya vijana wengi kushiriki kwenye kilimo lakini pia isaidie vijana kupata teknolojia ambazo zitawawezesha kulima kwa tija na kufurahia kilimo.

“Sisi kama chama tunaendelea kutoa elimu na kujenga uelewa wa pamoja kwa  umma kuhusu umuhimu wa bioteknolojia ya kisasa na manufaa yake katika uzalishaji duniani ili Serikali na watunga sera wabadili mitazamo yao na kuweka mazingira mazuri ya watafiti kufanya tafiti lakini pia mazao yake yaweze kufika sokoni” alieleza Prof. Msolla.

Amesema hoja zote zinazotolewa na wapinzani wa teknolojia hiyo hazina ushahidi huku wakiacha manufaa makubwa ya teknolojia hiyo kama vile kuzalisha mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya magonjwa,wadudu na mabdiliko ya tabia nchi, matumizi yake kwenye afya katika kutengenza chanjo na madawa pamoja na utunzaji wa mazingira na uzalishaji wa mbolea.

“Hapo nyuma kutokana na kelele nyingi za wapinga teknolojia hiyo walipelekea serikali kusitisha tafiti hizo hasa kweye kilimo lakini tunaishukuru serikali kupitia elimu kubwa iliyotolea na chama chetu kuamua kuruhusu watafiti waanze tafiti hizo kwa maslahi mapana na taifa” alisema Prof. Msolla.

Kwa upande Waziri wa Kilimo mstaafu na mmoja wa waanzislishi wa chama hicho Prof. Jumanne Maghembe amesema lengo la teknolojia hiyo ni kumsaidia mkulima kuzalisha kibiashara badala ya kuendela kuzalisha kwa kujikimu na kumfanya abaki palepale miaka yote akisongwa na changamoto nyingi za kilimo.

“Tumekuwa tikisikia wakipotosha kuwa mbegu za GMO zitawafanya wakulima wetu kuwa watumwa wa mbegu,mara wengine tutapoteza mbegu za asili haya yote majibu yake yapo wazi kuwa mbegu za asili haziwezi kupotea kwakuwa Tanzania ina benki ya mbegu zote za asili pale Arusha na kama utafuta kanuni bora za kilimo mazao unayovuna hayana sifa ya mbegu kwakuwa mbegu zina sifa zake hivyo haiwezi kumnyima mkulima kupanda tena mbegu hizo kama mbegu zingine” alifafanua Prof. Maghembe.

Chama cha bioteknolojia Tanzania (BST) Kilianzishwa mwaka 2016 kikiwa na wanachama 100 lakini sasa kimefikisha wanachama zaidi ya 450 ambao wanajumuisha, Watafiti, Wanasayansi, Wanasiasa,Wanafunzi, Wakulima, Wenye Viwanda, Wafugaji, Mashirika ya kiserikali na yansiyo ya kiserikali,Wanasheria na wadau wengine kutoka kila kona za Tanzania.
                    



 

No comments