Header Ads

test

TORITA KICHOCHEO CHA UZALISHAJI BORA WA TUMBAKU NA UCHUMI

Na: Calvin Gwabara – Tabora.


Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku nchini (TORITA) imechangai kuongeza mara dufu uzalishaji wa zao hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 na kuongeza ubora wa zao hilo, hivyo kuinua kipato cha wakulima na pato la Taifa hasa fedha za kigeni.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) Dkt. Jacob Bulenga Lisuma wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mchango wa taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake na mikakati waliyonayo katika kufikia malengo makubwa ya Kitaifa kuhusu zao hilo. 

“Taasisi yetu ya TORITA imetoa mchango mkubwa sana kwenye uzalishaji wa Tumbaku nchini ambapo mwaka jana 2022 tulizalisha mbegu bora nyingi na kuziuzia kampuni ambazo ziliweza kuzalisha tani milioni 125 tofauti na mwaka juzi ambapo uzaishaji ulikuwa tani milioni 65 tu” alieleza Dkt. Jacob.

Amesema ukifuatilia zao la Tumbaku kabla ya kuanzishwa kwa TORITA, kuanzia mwaka 2000 kurudi nyuma uzalishaji ulikuwa chini ya tani milioni 20. Baada ya mwaka 2000 uzalishaji ulianza kupanda na kuwa tani milioni 25, 35, 60, 85, 90 na hadi kufikia tani Milioni 125 za mwaka jana.

Amesema kuongezeka kwa uzalishaji huo kunatokana na mbegu bora walizozifanyia utafiti na kuzizalisha kwa wingi kupitia taasisi yao hasa baada ya kutoridhishwa  na uzalishaji haba katika eneo husika ambalo lilikuwa tatizo kwa wakulima wengi. Wengi wao uzalishaji wao ulikuwa ni mdogo kutokana na kulima kwa kutumia mbegu za asili na bila kufuata kanuni bora za kilimo cha Tumbaku. 

Juhudi za TORITA katika kuongeza uzalishaji zinachagizwa na ilani ya Chama Tawala na maelekezo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mathalani, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatutaka ifikapo mwaka 2025/2026 tuweze kufikia lengo la kuzalisha Tani milioni 200 za Tumbaku na ukiangalia msimu uliopita tulikuwa na tani milioni 125 hivyo bado tuna upungufu kidogo kufikia kiasi hicho ambacho tunaamini tutakifikia” Alifafanua Dkt. Jacob.

Mkurugenzi huyo wa TORITA ameishurkuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha za utafiti kwenye taasisi hiyo ambapo milioni 500 zilitumika mwaka wa kwanza kwenye kuzalisha mbegu bora za Tumbaku na kununua vifaa vya mabaara ambavyo vinasaidia kuhakikisha vinasaba vya mbegu bora vinachukuliwa ili kuzalisha mbegu bora na zenye sifa zinazohitajika pamoja na ununuzi wa trekta na magari mawili.

Aidha Dkt, Jacob amesema ni dhamira yao kuhakikisha wanasaidia kuongeza tija ya uzalishaji wa Tumbaku nchini kwakuwa ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo yameweza kutoa mchango mkubwa kwenye kuongeza pato la Wananchi na Taifa kwakuwa amaanini takwimu za mwaka huu zikitoka linaweza kuwa zao linaloongoza katika kuingiza fedha za kigeni.

Ametumia nafsi hiyo pia kuishukuru wizara ya Kilimo kupitia kwa Waziri wake Mhe. Hussein Bashe na mwenyekiti wa Bodi ya TORITA Prof. Gration Rwegasira (Wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo) kwa ushirikiano mkubwa wanautoa katika kuhakikisha Taasisi hiyo inafikia  malengo yake.
Mkurugenzi huyo amesema pia katika kufikia malengo ya Progamu ya BBT pia Taasisi yake imekuwa ikisaidia vijana wengi kuweza kuingia kwenye shughuli za kilimo ili ifikapo mwaka 2030 kilimo kiweze kuchangia asilimi 10 kwenye pato la taifa kupiti ajenda ya 2030.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa TORITA nchini, Prof. Gration Rwegasira wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo amesema, TORITA ni Taasisi ya Utafiti ambayo imejipanga vvema kutimiza malengo yake kama yalivyoainishwa katika mpango mkakati wa mwaka 2021-2026. 

Amesema kwakuwa TORITA iliasisiwa katika Misingi ya ushirikiano wa serikali na sekta binafsi yaani (Public Private partnership-PPP), imekuwa Taasisi ya mfano wa kuigwa ambayo inazingatia mahitaji ya Wakulima wakubwa na wadogo, Vyama vya ushirika wa Tumbaku, Makampuni ya ununuzi wa tumbaku na mifumo ya uendeshaji ya Serikali ili kuleta ufanisi na kuongeza pato la taifa.

 “Tunajivunia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya wadau za zao la tumbaku na Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania pamoja na Bodi ya Tumbaku ambao kwa pamoja wamewezesha kuimarisha uzalishaji wa zao hili na kuongeza tija kwa wakulima na kuinua pato la Taifa.” alisema Prof. Rwegasira.

Aidha Mwenyekiti huyo wa bodi ya itanabaisha kwamba, TORITA ni Taasisi pekee nchini ambayo  uongozi wake wa Bodi ya Wakurugenzi, pamoja na wadau wengine, unazingatia uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha kilimo (SUA) kama msingi mkuu wa kuhuisha utaalamu na teknolojia za kisasa kwa faida ya wakulima na umma wa watanzania. 

“Namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake yote hasa kupitia Wizara ya Kilimo, kwa jinsi wanavyothamini mchango wa TORITA na kuisaidia Taasisi kwa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi, lakini zaidi sana kwa sera nzuri na miongozo inayotuwezesha sisi Bodi ya Wakurugenzi wa TORITA kuisimamia vema Taasisi hii ili iweze kuwatumikia wakulima wa Tumbaku na wadau wake nchini Tanzania” alieleza Prof. Rwegasira. 

TORITA imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali zenye lengo la kuwasaidia wakulima kulima Tumbaku kitaalamu na kuongeza kiasi cha mazao yanayozalishwa katika kila eneo, tafiti za mbegu bora, rutuba ya udongo, visumbufu vya mimea, mbolea na teknolojia za ukaushaji tumbaku zinazozingatia misingi ya kuhifadhi mazingira.





 

No comments