Header Ads

test

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA AMEFANYA ZIARA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MNAZI MMOJA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefanya ziara katika Hospitali ya rufaa Mnazi Mmoja kufuatilia utoaji wa huduma hospitalini hapo.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed amepata fursa kutembelea huduma zinazotolewa katika Idara ya Uchunguzi, Idara ya upasuaji, kitengo cha Bima na wagonjwa wakulipia (First truck), na Idara ya kinga.

Ambapo ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ya kuwapatia wananchi huduma ya afya bure ili waweze kupata huduma hiyo ya Msingi bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Amesema hakuna sababu ya wagonjwa kupata tabu katika kufuata huduma ikiwemo Vipimo, vifaa na dawa huduma ambazo Serikali inatenga kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kugharamia upatikanaji wa huduma hizo.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote atakaemtoza fedha mgonjwa kwa ununuzi wa vifaa au kumtaka afanye malipo ili apate matibabu.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhishwa na huduma za Maabara zinazotolewa Hospitalini hapo kwa utayari wao wa kuwahudumia wagonjwa wanaofika kupata vipimo ambapo amewaahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka mazingira mazuri katika kitengo hicho ili wananchi wapate huduma bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Amesema uwepo wa mashine na vifaa vya kisasa pamoja na mazingira mazuri ya kufanyia kazi ni ushahidi wa wazi kuwa wananchi wanaofika kupata huduma hiyo hawatopata usumbufu wa aina yoyote ikiwa ni dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma za afya.

Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed ametembelea wodi ya Mifupa na kuwakagua wagonjwa waliolazwa wodini hapo pamoja na kujua namna wanavyopata huduma kutoka kwa wahudumu wa Afya.

Mhe.Hamed ameridhishwa kuowa tatizo la wagonjwa kukaa muda mrefu bila ya kupata huduma limepungua kwa kiasi kikubwa na kuwataka watendaji katika Wodi hiyo kuendelea kuhudumia kwa uharaka na umakini zaidi.

Aidha Mhe. Hemed amesikitishwa kuona wagonjwa walio wengi katika Wodi hiyo wanatokana na ajali za Bodaboboa hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuongeza juhudi ili kumaliza ajali za barabarani hasa Bodaboda.

Nae waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameeleza kuwa ziara hiyo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni moja kati ya njia bora ya kushajiisha uwajibikaji kwa watendaji wa Wizara hiyo.

Amesema ziara za viongozi mbali mbali katika Hospitali za Zanzibar zinaibua mambo yaliyofichikana yanayotokea kwa kutowajibika ipasavyo ambapo Waziri huyo ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.







No comments