Header Ads

test

WANAWAKE REA WATOA MAJIKO YANAYOTUMIA NISHATI SAFI NA SALAMA KWA WATU 118 MKOANI DODOMA

Na Mwandishi wetu Dodoma

Jumuia ya Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wametoa majiko yanayotumia nishati safi na salama kwa watu 118 ambao ni wakazi wa kijiji cha Zanka na Kigwe kama sehemu ya shamrashamra za Sikukuu ya Wanawake Duniani katika tukio ambalo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rose Senyamule.

Awali Mhe. Senyamule alisema matumizi ya mkaa na kuni kwa Wanawake wengi wa vijijni yamekuwa juu kwa sababu kadhaa ikiwemo uchumi, teknolojia duni na kukosekana kwa taarifa sahihi za matumizi ya nishati mbadala na kuwapongeza Jumuia ya Wanawake wa REA kuwasaidia Wanawake wenzao wa vijiji vya Zanka na Kigwe.

“Leo hii, Wanawake wenzetu wa REA wametoa majiko ambayo yanatumia nishati safi na salama ya kupikia katika vijiji vya Kigwe na Zanka ili kuwawezesha wananchi wa kaya maskini kupunguza gharama ya matumizi ya kuni na mkaa,” alikaririwa Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa, tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya tani milioni mbili za mkaa, zimekuwa zikitumika kwa mwaka kama nishati ya kupikia na kuleta athari kubwa za kimazingira kwa Wanawake ambao wanalazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta kuni.Aidha, alitoa rai kwa Wasambazaji wa majiko hayo, kushirikiana na Wafanyabiashara wa maeneo ya vijijini ili kuhakikisha kuwa majiko hayo na teknolojia kama hizo zinafika vijijini na kwa bei nafuu ili Wananchi wengi wayanunue na kuyatumia.

Mhe. Senyamule ameishukuru Jumuia ya Wanawake wa REA kwa kuchagua vijiji vya Mkoa wa Dodoma (Zanka na Kigwe) ili kutoa msaada huo na kuongeza kuwa Watu wengi watahamasika na kuanza kutumia majiko hayo kupitia Wanufaika hao 118.

“Nina Imani kubwa kuwa Watu wengi wataanza kutumia majiko haya na hatimaye tutatunza na kuhifadhi mazingira na wakati huo huo kumpa Mwanamke wa kijijini fursa ya kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali,” amemalizia Mkuu wa Mkoa.

Akizungumza kwa niaba ya Jumuia ya Wanawake wa REA, Mkurugenzi wa Uendelezaji Teknolojia na Masoko, Mhandisi Advera Mwijage amesema takribani shilingi milioni tano (5,400,000) zimetumika kugharamia ununuzi wa majiko hayo kwa Wanufaika 118.

Mhandisi Mwijage amesema, mgawanyo wa majiko hayo umezingatia makundi maalum ambayo ameyataja kuwa ni pamoja na: - Kundi la Kaya Maskini.

Majiko banifu yanayotumia mkaa na kuni, Wananchi kutoka kaya masikini katika kijiji cha Zanka, majiko 54 na kijiji cha Kigwe, majiko 36.

Ameongeza kuwa mgawanyo wa majiko ulilenga pia kundi la taasisi ambalo linajumuisha watu kutoka Sekta ya Elimu (Waalimu) Sekta ya Afya (Watoa huduma za Afya) na Viongozi wa Serikali wakiwemo (Viongozi wa vijijini, kata, Madiwani na Wasaidizi wa Mahakama) ambao wote kwa pamoja wamepewa seti ya jiko la gesi pamoja na mtungi wake.

Kwa upande wa kijiji cha Zanka, wanufaika ni 15 na kwa upande wa kijiji cha Kigwe ni wanufaika 13.

Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa lengo la Jumuia ya Wanawake wa REA lililowasukuma kuchanga fedha kutoka mifukoni mwao na kununua majiko ili wayagawe kwa Wanakijiji wa Zanka na Kigwe kwanza ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia vijijini.

Amesema nishati kubwa inayotumiwa na watu wengi vijijini hususani wanawake ni kuni na kuongeza kuwa msaada huo umelenga kwenye familia zenye uhitaji mkubwa.

“Tumegawa majiko yanayotumia mkaa kidogo na yanahifadhi joto, kuna kundi la watu ambao hawezi kuacha mara moja matumizi ya kuni, tunatoa majiko yanayotumia mkaa kidogo na kuni kidogo, unaweza kutumia kuni mbili tu na ukapika chakula cha familia nzima,” aliisitiza Mhandisi Advera.Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa changamoto za uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kumpunguzia mwanamke muda wa kutafuta kuni ili ashiriki kwenye shughuli nyingine za kiuchumi, zimewasukuma kuchanga fedha kwa ajili ya kununua majiko hayo na kuyagawa kwa familia hizo 118 za kijiji cha Zanka na Kigwe.

Aidha, amegusia kuwa REA kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wameanza kutekeleza Mradi wa kusambaza gesi asilia katika Mkoa wa Lindi na Pwani kwenye kaya zinazopitiwa na bomba la gesi asilia; Mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 23.Mradi mwingine ni wa kusambaza majiko bora kwa kaya zaidi ya 220,000 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akihutubia katika hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia nishati safi na salama katika kijiji cha Zanka
Hafla hiyo imeandaliwa na Jumuia ya Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Godwin Gondwe akihutubia kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule katika hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia nishati safi na salama katika kijiji cha Zanka Hafla hiyo imeandaliwa na Jumuia ya Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkurugenzi wa Uendelezaji Teknolojia na Masoko kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Advera Mwijage akihutubia katika hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia nishati safi na salama katika kijiji cha Zanka. Hafla hiyo imeandaliwa na Jumuia ya Wanawake wa REA.
Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akimkabidhi Mwenyekiti wa kijiji cha Kigwe, wilayani Bahi, (Jina lake) jiko la gesi na mtungi wake katika hafla iliyoandaliwa na Jumuia ya Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wengine wanaoshuhudia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Godwin Gondwe na kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mhandisi Advera Mwijage, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Teknolojia na Masoko kutoka REA.
Sehemu ya umati wa watu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akihutubia katika hafla ya kukabidhi majiko yanayotumia nishati safi na salama katika kijiji cha Zanka, wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma, Hafla hiyo iliandaliwa na Jumuia ya Wanawake wa REA.

No comments