Kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo yafanyika Iringa
Na: Genofeva Matemu – Iringa
03/04/2023 Wananchi wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kutumie fursa ya uwepo
wa madaktari bingwa wa moyo kujitokeza kwa wingi kuchunguza moyo kupitia
kambi maalum inayofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa
(IRRH) Dkt. Alfred Mwakalebela wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo inayofanyika
kwa siku tano lengo likiwa ni kufikisha huduma karibu kwa wananchi.
Dkt. Mwakalebela alisema kupitia kambi hiyo wananchi watapata fursa ya
kupimwa vipimo vyote vikubwa vya moyo, kupata dawa kwa wale watakaokutwa
na magonjwa ya moyo na wengine watakaohitaji uchunguzi zaidi watapewa rufaa
kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
“Tukipata wataalamu kama hawa katika Hospitali yetu kunasaidia kuwachunguza
kwa kina zaidi wagonjwa na baada ya hapo wataalam hawa watatuachia
wagonjwa hao kwa ajili ya kuendelea na kliniki hapa kwetu hivyo kupunguza tatizo
kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa awali”, alisema Mwakalebela.
Dkt. Mwakalebela alisema kupitia wataalam waliotoka JKCI wanaenda
kuwaonyesha njia wataalam wa IRRH ya namna ya kuwachunguza wagonjwa wa
moyo pamoja na kuwafuatilia mara kwa mara ili kwapamoja waweze kuwafuatilia
kwa karibu na kuwapa huduma stahiki.
“JKCI imekuwa na utaratibu wa kupeleka huduma karibu na wananchi ili waweze
kupata huduma kwa urahisi zaidi na sasa ni zamu yetu wananchi wa Mkoa wa
Iringa, tunaahidi kushirikiana nao kuwasaidia wananchi wetu”, alisema
Mwakalebela.
Kwa upande wake Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro
Pallagyo alisema magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio yanayoongoza kwa
kusababisha vifo vingi ulimwenguni na katika mazingira ya Tanzania magonjwa
hayo yanaonekana yakiongezeka kwa kasi.
“Wataalam wa JKCI tupo Iringa kwa ajili ya kufanya vipimo na huduma za kibingwa
za moyo hivyo tukiwa na utaratibu wa kuchunguza afya zetu na kugundua
mapema inakuwa rahisi kutibu na kuwa na matokeo mazuri zaidi”, alisema Dkt.
Pedro.
Dkt. Pedro alisema mwamko wa wananchi kuchunguza afya zao bado uko chini
lakini kupita kambi maalum za matibabu ya moyo wanazofanya toka wameanza
mwitikio umekuwa ukiongezeka huku lengo likiwa kuwasaidia wagonjwa na
kujenga desturi kwa watu kuwa wanachunguza afya zao mara kwa mara.
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Gerald Isambo alisema
amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kifua mara kwa mara na kutokupata utatuzi
nini kinachomsumbua hivyo kupitia kambi hiyo amepata fursa ya kupima moyo
wake.
Isambo alisema kuwa hakuwahi kupima moyo tangu kuzaliwa kwake hivyo fursa
hiyo aliyoipata imempa mwamko wa kufanya uchunguzi wa afya yake mara kwa
mara na kuacha tabia ya kuchuguza afya yake pale tu anapoumwa.
“Naomba kupitia Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa huduma kama hizi na
nyingine za kibingwa ziendelee kutolewa mara kwa mara kutupa nafasi sisi
wananchi ambao hatuwezi kuzifuata mahali zilipo kuchunguza afya zetu na kuwa
na desturi ya kujichunguza”, alisema Isambo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Elizabeth Meli akimpima shinikizo la damu mwilini (BP) raia wa Switzerland Lans Sottwals aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) leo kwa ajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya sikun tano inayofanywa na wataalam hao kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga akimfanyia utafiti mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) kwa ajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo leo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali hiyo. Kambi hiyo ya siku tano inafanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na
wenzao wa IRRH.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimwelezea mwananchi wa Iringa Imelda Harrison namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) kwa ajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo leo katika kambimmaalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akimfanyia mgonjwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) leo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Picha na: JKCI.
Post a Comment