SERIKALI IMEENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA
Picha ya Juu inavyoonekana katika Kijiji cha Misinge Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora inavyoonekana ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), mkoa wa Tabora Mhandisi Rwegoshora Michael akizungumza na Waandishi wa habari Juu ya mradi huo.
Mhandisi Mshauri wa Mradi Kazilambwa Chagu, Isaya Mosha akifafanua mafanikio na namna Barabara hiyo ilivyokuwa umuhimu kwa watu wa Tabora.
Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
SERIKALI imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi wa Miundombinu ya barabara inayojengwa katika mkoa wa Tabora ambao una jumla ya kilometa 2,188.09 za barabara zinazohudumiwa na wakala wa barabara TANROADS.
Miongoni mwa miradi ya barabara inayotekelezwa katika mkoa huo ni pamoja na kipande cha barabara cha Kazilambwa-Chagu ambao upo mbioni kukamika huku ukitengeneza ajira kwa vijana 400 mkoani humo.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kazilamwa hadi Chagu yenye urefu wa kilometa 36 kunatajwa kuwezesha shughuli mbalimbali za usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya nchi ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa Aprili 19, 2023 na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Rwegoshora Michael wakati ziara yake ya kutembelea mradi huo kuona maendeleo ya utekelezaji ambapo amesema, hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 89.62.
Mhandisi Rwegoshora ameendelea kwa kusema kuwa, mradi unaotekelezwa na mkandarsi STECOL Corporation chini ya mhandisi mshauri TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU) ambapo ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali yake ikiwemo kutoa fedha za utekelezaji wa miradi pamoja na kuwalipa wakandarasi wanaotekeleza miradi ikiwemo miradi ya ujenzi barabara kwa wakati.
"TANROADS Mkoa wa Tabora tunaishukuru na kupongeza serikali ya awamu sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa inazozifanya ili kukamilisha malipo ya wakandarasi ikiwemo mkandarsi wa mradi huu, mkandarsi wa mradi huu (STECOL) analipwa kwa wakati" alisema mhandisi Rwegoshora
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhandisi Mshauri kutoka TANROADS Engineering Consulting Unit, Mhandisi Isaya Mosha ameeleza kuwa, barabara ya Kazilamwa-Chagu ina urefu wa kilometa 36 ambapo kilometa 26 ziko katika Mkoa wa Tabora na kilometa 10 ziko katika Mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa, kama mhandisi mshauri anapata furaha kuona wanaelekea kukamilisha mradi huo.
Vilevile Mhandisi Mosha amesema, kama mkandarsi mshauri wataendelea kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kujiridhisha viwango stahiki kulingana na vigezo vya muda na mkataba.
"Tunajiridhisha kwa kiwango kinachostahili kutokana na mkataba, kwamba kazi inafanyika kwa kiwango kinachostahili" alisema Mhandisi Mosha na kuongeza kuwa
"Manufaa ya mradi huu ni pamoja na kutoa fursa za ajira kwa zaidi ya watu 400, kuchimba visima vitano na kuboresha baadhi ya barabara za michepuko kutoka katika barabara kuu zinazoelekea katika maeneo yanayopatikana huduma mbalimbali za kijamii"
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, Kaimu Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Ngoko Mirumbe amesema, kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma kwenda mikoa ya jirani ikiwemo Tabora au kwenda mikoa ya mbali ikiwemo Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya shughuli za biashara.
"Kukamilika kwa barabara hii ni fursa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma kufika kwa wakati katika mikoa ya Tabora, Dar es Salaam na mikoa mingine nchini" alisema Mhandisi Mirumbe
Akielezea hali ilivyokuwa hapo zamani, Mhandisi Mirumbe amebainisha kuwa, awali watu wa Mkoa wa Kigoma walikuwa wakisafiri kuelekea Mkoa wa Dar es Salaam kupitia Nyakanazi lakini sasa wanasafiri kupitia ya Tabora ambapo zaidi ya kilometa 300 zimepungua na hivyo kupunguza gharama za usafiri na kuokoa wakati ambao ulikuwa ukipotea barabarani wakitumia njia ya Nyakanazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Ugansa wilayani Kaliua, Anastazia Robert, Adide Matongo, Mohammed Seleman na Arasul Maftaha wameeleza changamoto mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo kabla ya ujenzi wa barabara hiyo ikiwemo barabara hiyo kutopitika nyakati za mvua, changamoto ya kupata usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ambapo sasa changamoto hizo zikigeuka historia ambapo hawakusita kutoa shukrani kwa serikali ya awamu sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujio wa mradi huo uliochochea ukuaji wa uchumi na kuibua fursa za kiuchumi ikiwemo biashara maeneo ambayo barabara hiyo inapita.
Miradi ya ujenzi wa barabara yenye jumla ya kilometa 238. 9 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 321 imetekelezwa mkoani Tabora. Kati ya miradi hiyo ni mradi mmoja ndio bado unaendelea kutekelezwa na umefikia asilimia 89.62 ambao ni mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Kazilamwa-Chagu (KM 36), jambo ambalo linatajwa kuwa ni hatua na maendeleo makubwa katika ngazi ya mkoa.
Post a Comment