Tumia hii Tafadhali: TMDA KANDA YA KATI YATOA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA MKOANI SINGIDA
Na Dotto
Mwaibale, Singida
MAMLAKA ya Dawa
na Vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Kati imetoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba pamoja
na vitendanishi kwa makundi mbalimbali
ya kijamii na wanafunzi Mkoa wa Singida ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea
kutokana na utumiaji wa dawa hizo kiholela.
Akizungumza na
waandishi wa habari wakati wa utoaji wa mafunzo hayo Afisa Mwandamizi Elimu
kwa Umma wa TMDA Kanda ya Kati, James Ndege alisema mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu hiyo
pamoja na kujifunza kutoa taarifa ya madhara yanayotokana na matumizi ya bidhaa hizo.
Alisema matumizi
yasiyo sahihi ya dawa na vifaa tiba na vitendanishi yanasababisha athari kubwa
kwa watumiaji, watu kupoteza maisha,kupata ulemavu na viungo mbalimbali
kuathirika kama ini na , figo.
Ndege alisema
elimu hiyo ni muendelezo ili wananchi waweze kujua namna bora ya matumizi ya
dawa na ndio maana wameanzisha klabu katika shule mbalimbali ili elimu hiyo
inayotolewa na TMDA iweze kusambaa kila maeneo na kuifanya jamii kuelewa athari
za matumizi ya dawa hizo.
Aidha Ndege
alitoa wito kwa wananchi kuzingatia
matumizi sahihi ya dawa ikiwemo kuepuka matumizi holela ya dawa kwa kutumia
dozi kikamilifu sambamba na kupata vipimo na ushauri wa wataalam wa Afya kabla
ya kutumia dawa hizo.
Alisema kuna changamoto kubwa kwenye jamii ya
watanzania kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia dawa wanapojisikia kuumwa bila kupima wala
kupata ushauri wa daktari na kwamba wengi wao zimewapelekea kupata madhara
kiafya.
"Kuna changamoto kubwa katika jamii kwa watu
kutumia dawa kiholela na sisi TMDA tunaendelea kuwaelimisha kuwa utumiaji wa
dawa kiholela unaweza kusababisha usugu wa bakteria na kufanya dawa hizo
kushindwa kufanyakazi kama inavyotakiwa" alisema Ndege.
Pia Ndege aliwataka wananchi kuzingatia muda wa
kutumia dawa hizo kama walivyoelekezwa na madaktari kwani kutumia dawa hizo kwa
muda ambao hawajaelezwa zinaweza kuwaletea changamoto za kiafya.
Aidha alitoa angalizo kwa wanafunzi wasichana kuacha ama kutojiingiza katika matumizi ya dawa za dharura za kuzuia mimba hasa
katika wakati huu ambao wapo shuleni na umri mdogo na kuwa matumizi ya dawa
hizo zinaweza kuwa na athari kubwa kwao za mfumo wa uzazi pindi wakiwa watu wazima na umri unaoruhusiwa kufunga ndoa au kupata watoto.
Ndege pia alitoa angalizo hilo kwa wanafunzi
wavulana nao kuacha kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambapo nao wanaweza
kupata athari zilezile ambazo zinaweza kuwapata wasichana na badala yake
aliwataka kusoma kwa bidii na kufanya mazoezi hali itakayowasaidia kutowaza
kufanya ngono.
Katika mafunzo hayo waliweza kuzindua klabu
zilizoanzishwa na TMDA katika shule mbali kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu
matumizi yasiyo sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi na masuala yote
yasiyo salama ya matumizi ya dawa hizo.
Shule ambazo zimepatiwa mafunzo hayo hadi leo May 4, 2023 ni shule sita za sekondari za Kindai, Dk. Salmin, Ipembe, Senge Singida, Utemini na wananchi wa Kata za Mitunduruni, Majengo na Mungumaji zote za Manispaa ya Singida..
Post a Comment