PROF. JAY: HALI YANGU ILIKUWA MBAYA SANA ISIYOELEZEKA
-Amshukuru Rais Samia
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Msanii wa Muziki nchini Tanzania, Joseph Haule maarufu Prof. Jay amejitokeza hadharani na kuwashukuru Watanzania baada ya Afya yake kuimarika ikiwa ni muda mrefu tangu atoke kwenye maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
Prof. Jay ametoa shukrani hizo kupitia ukurasa wake wa ‘Instagram’ huku akimshukuru Mwenyezi Mungu baada ya Afya yake kuimarika, Prof. Jay amemshukuru pia Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake anayoongoza.
“Kwanza namshukuru sana MUNGU aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, Hali yangu ilikuwa mbaya isioelezeka, Asante sana Mungu baba (nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu).”
“Pili Kipekee namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Dkt. Samia Hassan Suluhu na Serikali yake kwa kunigharamia matibabu yangu yote ya Muhimbili na nje ya nchi, ahsante sana Mama pamoja na serikali yako yote kwani viongozi wako wa chama na serikali walikuwa wanapishana kila siku kuja kuniona na kunifariji,” ameandika Prof. Jay
Aidha, Prof. Jay amemshuru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe sanjari na Viongozi wengine kwa jitihada zao za kuhakikisha wananusuru maisha yake kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
“Mwisho na kwa umuhimu mkubwa sana nawashukuru sana Watanzania wote mliojitolea kwa maombi na michango ya fedha zenu kuhakikisha natibiwa na kusema ukweli ilinisaidia sana kulipa bills za awali kabla ya serikali kuamua kuingilia kati na kuubeba mzigo huu asanteni sana na sitowasahau.”
“Nitakuwa mchoyo wa Fadhila nisipoishukuru Familia yangu Mke wangu, Kaka zangu, Dada zangu Wadogo zangu na Familia yote ya Mzee Haule kwa ushirikiano mkubwa na upendo mliomipa. Kwa sasa nipo imara na ninaendelea vizuri sana Mungu ni mwema sana siku zote.”
Kwa takribani mwaka mmoja uliopita, hali ya kiafya ya Prof. Jay iliripotiwa kuwa si shwari na alikuwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Post a Comment