SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI YA TREES FOR THE FUTURE
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson (katikati waliokaa mbele) akiwa na viongozi wengine, kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kimataifa ya Trees for the Future Tanzania, Heri Rashid na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga pamoja na wakulima waliohitimu mafunzo ya kilimo mseto yaliyotolewa na Taasisi hiyo. Katika mahafali hayo yaliyofanyika Kata ya Siuyu May 5, 2023 wahitimu hao walitunukiwa vyeti na zawadi mbalimbali. Kushoto walio simama nyuma ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe na Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovison Ntangeki.
Na Dotto Mwaibale,
Singida
SERIKALI imesema
itaendelea kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya kimataifa ya Trees for the
Future Tanzania inayojishughulisha na kilimo mseto, kilimo endelevu kwa
wakulima wenye kipato cha chini vijijini ili kutokomeza njaa, Umaskini na Ukataji
wa miti, yenye makao yake makuu mkoani Singida ambayo inatekeleza mradi wa Bustani
Misitu.
Hayo yamesemwa na
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba katika mahafali ya wakulima 1445
waliohitimu mafunzo ya utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu katika Wilaya ya Ikungi.
"Serikali
itaendelea kushirikiana na taasisi ya Trees for future kwani imekuwa na mchango
mkubwa wa kusaidia wakulima hapa mkoani kwetu hasa katika uhifadhi wa
mazingira na kilimo mseto ambacho kina wasaidiawananchi kupata chakula na mbogamboga" alisema Serukamba.
Aidha, Serukamba
aliwataka wananchi mkoani hapa kupanda miti katika maeneo ya kuzunguka nyumba
zao na kwenye kingo za barabara na maeneo yote ya taasisi za Serikali ikiwa ni kuunga
mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za utunzaji wa mazingira na
kuhifadhi vyanzo vya maji.
Mkurugenzi wa
taasisi hiyo, Heri Rashid akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa alisema taasisi hiyo
imepanda miti ya matunda, mbao, uzio na miti ya kurutubisha udongo na kwamba
ifikapo 2030 malengo yao ni kupanda miti bilioni moja.
Alisema miti hiyo
ina manufaa makubwa kwa mazingira ikiwa ni pamoja na kufyonza hewa ukaa na
kuzalisha hewa safi na inasaidia katika kupambana na mabadiliko ya tabia ya
nchi.
Rashid alisema mradi
wa Bustani Msitu umekuwa chanzo cha vyakula vya aina mbalimbali vyenye lishe
kwa kaya 1445 za wahitimu kupitia upandaji wa mbogamboga na miti ya matunda.
"Wakati
tunaanza utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu wanufaika wetu walikuwa chini ya
asilimia 25 tu ambao ndio walikuwa na uwezo wa kupata matunda na mbogamboga
lakini hivi sasa wanufaika wapo zaidi ya asilimia 83 ambao wanapata mbogamboga
na matunda ndani ya saa 48," alisema.
Alisema kupitia
mradi huo ambao lengo kuu ni kuongeza uzalishaji katika shamba la mkulima,
wakulima wameweza kuuza matunda yao sokoni mjini Singida kama vile pasheni na
papai na hivyo kujipatia fedha ambazo zimewasaidia kuendesha maisha yao ya kila
siku.
Aliongeza kuwa baada
ya wakulima kuanza kunufaika na bustani zao, taasisi ya Trees for the future
ilianzisha vikundi 107 vya wakulima vya huduma ndogo za fedha ambavyo
vimesajili katika halmashauri za Wilaya ya Singida, Mkalama,Iramba na Ikungi.
Alisema vikundi
hivyo vinawasaidia wakulima kuweka akiba na kulipa ili fedha zinazopatikana
kutoka kwenye mazao ya Bustani msitu iweze kuzungushwa miongoni mwa wakulima
wanufaika hali ambayo imesaidia kuinua hali zo za maisha.
Alisema pamoja na
mafanikio yaliyopatikana kumekuwa na changamoto ya tatizo la ukame kutokana na
ukanda huu kupata mvua chache, mifugo kuchungiwa kwenye mashamba ya Bustani
msitu na upungufu wa fedha za kuendesha miradi.
Mnufaika wa mradi
huo Juma Shabani ameishukuru taasisi hiyo kwa kumpa maendeleo katika kilimo
hadi kufikia hatua ya kuingiza umeme na maji kwenye nyumba yake aliyoijenga
Kata ya Mungaa.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga aliiomba taasisi hiyo kuongeza
miaka mingine ya kutekeleza mradi wa namna hiyo kwenye wilaya hiyo ili wananchi
wengi waweze kunufaika na teknolojia hiyo ya uhifadhi wa mazingira pamoja na
kilimo mseto.
Kabla ya kuanza kwa
mahafali hayo RC Serukamba aliyekuwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa na wataalam mbalimbali alipata fursa ya kutembea mashamba ya wanufaika wa
mradi huo, Basili Mtaturu na Juma Shabani yaliyopo Kata ya Mungaa na Siuyu ambapo alijionea kazi kubwa
iliyofanyika ya utunzaji wa mazingira kupitia kilimo mseto.
Post a Comment