Header Ads

test

DKT, ABBASI - TOUR GUIDE MNA DHAMANA KUBWA KWENYE UTALII

 


Na John Mapepele

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amefunga mafunzo maalum ya siku nne ya uongozaji wa utalii kwa zaidi ya Waongoza Utalii 1300 kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa yaliyoratibiwa na Hifadhi za Taifa (TANAPA) huku akiwataka kuzingatia utaalam wa fani ya uongozaji wa utalii ili kuboresha huduma kwa watalii na kuwavutia kuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.


Dkt. Abbasi amefunga mafunzo hayo jijini Arusha leo Aprili 30, 2023 huku akisisitiza kuwa waongoza utalii ni nguzo muhimu katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Utalii ambapo amesisitiza kuwa wanadhamana kubwa ya kuhakisha huduma inatolewa kwa kiwango cha kimataifa ili kuwafanya watalii kutoka maeneo mbalimbali kurejea mara kwa mara nchini hatimaye kukuza vipato vyao na uchumi wa Taifa kwa ujumla.


“Ndugu zangu hapa naomba niseme tu kuwa sisi waongoza utalii ndiyo watu ambao tunaweza tukawafanya wageni waendelee kuja kutuletea fedha ama la hivyo nitoe wito kwenu kuona kwamba kazi yenu ni ya thamani kubwa katika taifa letu ndiyo maana hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano alitoka ofisini akacheza filamu ya Royal tour kwa kutambua thamani ya uongozaji utalii, acheni kulia lia”. Amefafanua Dkt. Abbasi
Aidha, amesema waongoza utalii wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuwa wao ni watu wa kawaida na badala yake kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi raslimali zilizopo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye pia kuutangaza utalii.


“Katika kipindi cha sasa dhamira ya serikali inakwenda kujikita katika nguzo mbili kubwa kuhifadhi na kutangaza kwa nguvu zote vivutio mbalimbali vya utalii ambayo nchi yetu imebarikiwa kuwa navyo kila kona”. Amesisitiza Dkt. Abbasi

Akimkaribisha Dkt. Abbasi kufunga mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa TANAPA, William Mwakilema amesema semina hiyo imeratibiwa ili kuwajengea uwezo waongoza utalii wakati huu msimu wa utalii unavyoanza kufunguka ili wageni wanapofika waweze kupatiwa huduma bora.

Aidha amesema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa kwenye mafunzo hayo ni pamoja na wajibu wa waongoza utalii, changamoto za utalii katika vivuko vya Nyumbu Mto Mara Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ifahamu Mkomazi na uewekezaji kupitia mfuko wa Umoja Trust Fund kwa waongoza utalii.
Amesema kwa sasa mpango wa TANAPA ni kufungua mbuga na hifadhi tano zaidi ili nazo zijulikane kama zile kongwe, ambapo amezitaja hifadhi hizo kuwa ni Mkomazi ambayo itatangazwa kwa kauli mbiu ijulikanayo kama Discover Mkomazi, Sadani, Mikumi,Ruaha na Nyerere.

Akisoma risala kwa niaba ya waongoza utalii wote Ridas Michael Laizer ameiomba Serikali pamoja na mambo mengine kuwasaidia waongoza utalii kupatiwa bima ya afya ambapo Katibu Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kukaa chini na viongozi wa waongoza utalii kujadili kwa kina changamoto zote na kuzipatia ufumbuzi katika kiopindi kifupi ambapo pia amesisitiza kuwa viongozi wakuu wa Wizara wanazungumza na kujadiliana kwa kina na kila kundi kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Utalii ili kuendeleza sekta.

No comments