WAAJIRI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUJISAJILI NA KUWASILISHA MICHANGO WCF
NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MWANZA
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ametoa
wito kwa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF) kwa manufaa ya wafanyakazi pindi watakapopata changamoto za
kuumia au kuugua kutokana na kazi.
Ameyasema hayo Mei 22, 2023 katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla
wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu uliosababishwa na
ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa madaktari wa mikoa ya kanda ya Ziwa ikijumuisha
Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga katika ukumbi wa chuo cha BoT
jijini Mwnaza.
“Ili uweze kunufaika na huduma au mafao
yanayotolewa na WCF, ni lazima waajiri wajisajili na kuwasilisha michango ya
wafanyakazi waliowaajiri.” Alifafanua.
Alisema hivi sasa wafanyakazi wanao uhakika wa
kinga na kipato kutokana na majanga yanayosababishwa na ajali, magonjwa na vifo
kutokana na kazi kufuatia uwepo wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF).
“Waajiri nao wanapata muda zaidi wa
kushughulikia uzalishaji na uendelevu wa biashara zao na hivyo kuongeza tija
inayopelekea kuongezeka kwa pato la taifa.” Alisema.
Aliwaasa washiriki kuwa waadilifu
wanapotekeleza jukumu hilo la kufanya tathmini ya ulemavu utokanao na ajali au
magonjwa yatokanayo na kazi ili WCF iweze kutoa fidia stahiki na kwa wakati.
Alisema uwepo wa Mfuko wa Fidia ni hatua
muafaka katika mazingira ya sasa ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya
uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inaendelea na kazi ikiwemo ya kujenga uchumi na hivyo kuwa na ongezeko
kubwa la maeneo ya uzalishaji.
“Katika hali ya kawaida ongezeko litakwenda
sambamba na ongezeko la matukio na athari zinazotokana na ajali na magonjwa
yatokanayo na kazi hivyo jukumu la WCF sio kulipa fidia pekee bali pia
kushirikiana na wadau katika kubuni na kuendeleza mbinu za kupunguza au kuzuia
ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.” Alisisitiza.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu
wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema mafunzo
hayo ni sehemu ya hatua muhimu ya kuuwezesha Mfuko kutekeleza vyema jukumu la
kufanya tathmini sahihi na hatimaye kutoa fidia stahiki pindi mfanyakazi
anapoumia au kuugua kutokana na kazi.
“Katika mwaka huu wa fedha tayari tumetoa
mafunzo kwa madaktari 85 na leo tunawafundisha madaktari 100 na hivyo watafanya
idadi ya madaktari ambao tayari wamepatiwa mafunzo na WCF, ya kufanya tathmini
za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,585 nchi
nzima.”Alifafanua Dkt. Omar.
Akielezea zaidi umuhimu wa mafunzo hayo, Dkt.
Omar alidokeza kuwa Madaktari ni kiungo muhimu, ni daraja baina ya Mfuko na
wahanga wanaopata magonjwa au ajali zinazotokana na kazi.
“Madaktari hawa wakijengewa uelewa wa kuweza
kujua na kubaini magonjwa yanayotokana na kazi, vilevile wakaweza kufanya
tathmini za ulemavu, itawawezesha hawa wahanga kupata haki zao za fidia kwa
wakati lakini kupata stahiki zao.” Alisisitiza.
Kwa upande wa madaktari wameishukuru Serikali
kwa kuuwezwesha Mfuko kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na
kuwapatia mafunzo.
“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya
yatatuwezesha kufanya majukumu yetu ya kuwahudumia wafanyakazi watakaopata
changamoto za kuumia na au ulemavu kutokana na ajali na magonwja yatokanayo na
kazi kwa usahihi zaidi>” Alsiema Dkt. Pasclates Ijumba kutoka Hospitali ya
Rufaa Mkoa wa Geita.
Aidha Dkt.Julieth Nkovabi kutopka Hospitali ya
Bugando, alisema mbali na kupatiwa mafunzo hayo ya tathmini za ulemavu na
magonwja yatokanayo na kazi, lakini pia wamepatiwa elimu ya uelewa wa namna ya
kuwasilisha taarifa endapo mfanyakazi ataumia au kuugua.
“Na sisi watumishi wa afya tunakumbana na shida
mbalimbali, magonjwa ya kuambukiza wakati tunapowatibu wagonjwa wetu, kwa hivyo
ni fursa nzuri ya kuelewa hatua kwa hatua jinsi ya kuwasilisha taarifa.”
Alisema.
Post a Comment