TAASISI YA PROFESSOR MWERA FOUNDATION YAWAOMBA WALIMU SINGIDA KUANZISHA MFUKO WA ELIMU
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKURUGENZI
wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani
Mara, Hezbon Mwera amewaomba walimu Mkoa wa Singida kuanzisha mfuko wa elimu ambao
utasaidia kwa shughuli mbalimbali katika sekta ya elimu.
Mwera alitoa ombi hilo jana wakati akizungumza na walimu
hao kwenye mkutano wa wadau wa elimu mkoa wa Singida wa mwaka 2023 uliofanyika Aprili 27, 2023, Ukumbi wa Social
Mission mjini hapa.
“Nashauri kila halmshauri za mkoa wa Singida kwa
kuwashirikisha wadau wengine anzisheni mfuko wa elimu ambao utakuwa ukisaidia
kuboresha masualayote yanayohusu elimu katika maeneo hayo na mkoa wa Singida
kwa ujumla,” alisema Mwera.
Akizungumzia suala la upatikanaji wa chakula
mashuleni alisema jambo hilo linawezekana kwa kuwashirikisha wazazi na kuwa
maeneo mengine wameanza kwa kutoa uji na kueleza watoto wanapopata chakula
wanafanya vizuri katika masomo yao.
Alisema iwapo wataona wazazi hawatoi ushirikiano
katika jambo hilo ni vema siku moja wakaitisha kikao na wawashindishe njaa kuanzia asubuhi hadi
jioni hapo ndipo watakapoona umuhimu wa watoto kupata chakula wakiwa shuleni
kwani wapo ambao hawalielewi wakidhani linafanywa na Serikali.
.
Pia Mwera aliomba walimu kutoka vyuo vya ualimu
Mkoa wa Singida wanapo kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo ni vizuri wakafanya
mafunzo hayo kwenye shule za mkoani hapa na hata wakati wa likizo wawe wanafanya
hivyo na kuwa itaongeza ufaulu kwa wanafunzi kutokana na walimu hao kuwa na moto wa kufundisha..
Halikadharika, Mwera alisema ili kusaidia
wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kuongeza ufaulu ni kuanzishwa
vituo vya vijana kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata hadi Tarafa ambavyo vitakuwa na mashine
zitakazo tumika kudurufu mitihani itakayotumika kwa ajili ya kujifunza vijana
hao.
Katika mkutano huo Mwera alipata fursa ya
kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo kuwa ni pamoja na
kutoa mafunzo ya ufundi bure kwa vijana
ambapo kwa Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara zaidi ya Sh.Bilioni 3 taasisi hiyo
ingezipata iwapo kama ingehitaji kutoa mafunzo hayo kwa kutoza fedha na kuwa vijana
3500 wamenufaika.
Alitaja kazi nyingine ni kuhamasisha vijana wa
shule za msingi na sekondari kujiunga na vyuo vya ufundi baada ya kuhitimu,
kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya hoteli na utalii kwa kuhamasisha utalii
wa ndani pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake na
kuhamasisha watoto wa kike juu ya umuhimu wa shule.
Pia Mwera alisema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia watoto Yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kupata masomo kuanzia shule ya msingi, Sekondari hadi vyuo vya ufundi.
Alisema taasisi hiyo awali ilikuwa ikifanya kazi
katika mikoa 10 lakini kutokana na kufanya vizuri Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa kibali kuendelea kufanya kazi katika
mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo ameomba
maofisa wao watakapokuwa wakipita mikoani wapewe ushirikiano.
Hivi karibuni taasisi hiyo ya Mkoa wa Mara inayojishughulisha na masuala ya elimu ili mtunuku tuzo ya heshima Rais Dk.. Samia Suluhu Hassan kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini, tuzo aliyokabidhiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa niaba yake.
Post a Comment