Header Ads

test

VIONGOZI KATA YA ITIGI SINGIDA WAKUTANA NA MABALOZI KATIKA KIKAO KAZI

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itigi, Benjamin Masangula, akizungumza na mabalozi wa kata hiyo katika kikao kazi kilichofanyika juzi mjini humo. Wengine waliokaa meza kuu kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Samson Sirilo na Diwani wa Kata hiyo, Ally Minja.

...........................................

Na Dotto Mwaibale, Itigi 

VIONGOZI wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Kata ya Itigi mkoani Singida wamekutana na mabalozi wa kata hiyo kwa ajili ya kupanga mikakati ya utendaji wa kazi ili kuendelea kuisukuma mbele kata hiyo kimaendeleo.

Akizungumza katika kikao kazi hicho, Afisa Mtendaji wa kata hiyo Saimon Sirilo alisema wamekutana na mabalozi 56 wa Kata ya Itigi mjini ili kupanga mikakati nao ya kusukuma maendeleo ya kichama na Serikali.

" Mabalozi ni kundi muhimu sana katika jamii hasa katika kutekeleza majukumu ya chama na Serikali kutokana na kuwa jirani na wananchi tofauti na makundi mengine," alisema Sirilo.

Alisema pamoja na kukao nao katika kikao hicho lengo kubwa lilikuwa ni kuwatia moyo kutokana na mchango wao mkubwa katika jamii ili waendelee kuwa na ari na moto wakuchapa kazi kutokana na kutegemewa na chama, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Katibu wa CCM wa Kata hiyo, Benjamin Masangula akizungumza kwenye mkutano huo alisema kundi hilo la mabalozi ni la muhimu kwani wamekuwa wakichochea maendeleo ya wananchi katika nyanja zote mbili za kisiasa na Serikali na kwa kulitambua hilo wameamua kuwalipia  ada za uanachama mabalozi wote 56 kwa mwaka mzima.

"Mchango wa kundi hili ni mkubwa sana hatuwezi kuwatenga, chama na Serikali ni kama ulimi na mate tumeamua kuwatia moyo kwa kuwalipia ada za uanachama jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wetu," alisema Masangula.

Aidha, Masangula alisema wametoa kadi 100 ambazo zimetolewa kwa mabalozi hao kwa ajili ya kwenda kuwatafuta wanachama wapya wa chama hicho katika maeneo wanayotoka na kuwa mpango huo utakuwa ni endelevu wenye lengo la kukihimarisha chama kwa kupata wanachama wengi zaidi.

Katika mkutano huo viongozi wengine waliohudhuri ni Diwani wa Kata ya Itigi, Ally Minja ambaye aliomba kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya Serikali, chama na kundi hilo la mabalozi kwa mustakabari mzima wa maendeleo ya kata hiyo.

"Maendeleo ya kata yetu yataendelea kuwa juu iwapo tutadumisha upendo, mshikamo na kushirikiana sisi sote pamoja na wananchi wetu tunaowaongoza na si vinginevyo," alisema Minja 

Diwani wa Kata ya Itigi, Ally Minja akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Katibu wa CCM wa kata hiyo, Benjamin Masangula, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Taswira ya kikao hicho.
 

No comments