Header Ads

test

JAMII IENDELEE KUJIANDAA NA KUJIKINGA NA MAAFA- DKT YONAZI

Na; Mwandishi Wetu - Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameitaka jamii kujiandaa kila wakati ili kujikinga na maafa.
Ameyasema hayo mapema Leo Juni 30, 2023 Jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja,

Dkt. Yonazi alisema kuwa, Tanzania kama Nchi imepitia historia ya kukabiliwa na matukio ya maafa yatokanayo na majanga na milipuko ya magonjwa ya binadamu na Wanyama hivyo ipo haja ya kuwa na mipango ya kitaifa inayoratibiwa vyema kuwezesha kubaini viashiria na kushirikishana taarifa ili kuzuia maafa yanayoweza kutokea.

Pia alibainisha kuwa, Ufuatiliaji wa matukio yanayoweza kuathiri afya ya binadamu, wanyama na mazingira unatakiwa kufanyika kwa ufanisi kwa kuzingatia dhana ya Afya Moja kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja 2022 - 2023.

Dkt. Yonazi alisema, matukio hayo hutokea bila matarajio na huhitaji utambuzi wa mapema na kuchukua hatua za haraka za kukabili.

“Tumejifunza kuwa ili kudhibiti matukio hayo, hatuna budi kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na uratibu ili kudhibiti viashiria vya matukio yanayoweza kusababisha maafa kwa wakati.” Alisisitiza
Alitumia fursa hiyo kuhimiza watendaji kujifunza kutoka kwa Nchi zilizoendelea katika mifumo ya aina hiyo kwa lengo la kuboresha masuala ya menejimenti ya maafa.

“Nimefurahi sana kuona kuwa kuna washiriki kutoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali,na wawakilishi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, na kwa kuwa hili ni toleo la kwanza, sasa nitoe wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kuwa katika nchi zote zilizoendelea hawa ndo wabeba mwenge wa Sayansi na Teknolojia, tafiti zinafanywa katika majeshi na baaada ya hapo huamishwa na hupelekwa katika matumizi mengineyo.” Alibainisha Dkt. Yonazi.

Sambamba na hilo alitoa wito kwa Vyuo vya Elimu ya Juu hususan Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuendelea kutoa ushirikiano katika mtazamo wa kisayansi katika mambo yanayotatiza jamii na kuyatafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo,(SUA) Profesa Raphael Chibunda, Makamu alisema mradi huo wa kuanzishwa kwa jukwaa shirikishi la kidijitali ulizunduliwa mwaka 2022,na kupitia mradi huu shughuli mbali mbali zimetekelezwa,na ili kuhakikisha kituo hiki kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa ambapo Chuo cha (SUA) kilitoa vifaa vya TEHAMA vya Mradi huo vyenye thamani ya shilingi milioni 42.3.

Awali akitoa taarifa ya Mradi huo, Afisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Alex Ndimbo alisema lengo la kuanzishwa kwa jukwa hili ni kuongeza wigo kwa Jamii kutoa Taarifa kwa mamlaka husika.

“Jukwaa hili linawakutanisha wataalam wote ambao wanasimamia sekta zinazohusiana na wanyama, binadamu na mazingira wakikutana pamoja na kuratibu tutapunguza matukio ambayo yataleta majanga katika Taifa letu, mfumo huu unaenda kuruhusu wananchi wa kawaida kabisa kutoa taarifa kwa Serikali au Idara husika moja kwa moja kutoka katika eneo la tukio kupitia namba 190 kwa baadhi ya mitandao ya simu,” Alieleza.Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizindua Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na namba ya dharura ya kupokea taarifa za maafa Juni 30, 2023 Jijini Dodoma.



Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na namba ya dharura ya kupokea taarifa za maafa Juni 30, 2023 Jijini Dodoma.
Washiriki wa Hafla ya  Uzinduzi wa Jukwaa  Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na  namba ya dharura ya kupokea  taarifa za maafa wakiafuatilia matukio mbalimbali katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri  Mkuu  Juni 30, 2023 Jijini Dodoma.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda akifafanua jambo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na namba ya dharura ya kupokea taarifa za maafa wakiafuatilia matukio mbalimbali katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Juni 30, 2023 Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa hafla ya Uzinduzi wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na namba ya dharura ya kupokea taarifa za maafa uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Juni 30, 2023 Jijini Dodoma.
Afisa TEHAMA Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Alex Ndimbo akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (hayupo pichani) kuhusu mfumo wa Jukwaa Shirikishi la Mawasiliano ya Kidijitali la Afya Moja na namba ya dharura ya kupokea taarifa za maafa unavyofanya kazi.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments