RAS SINGIDA: SUALA LA KULETA MAENDELEO SIO LA RAIS PEKEE YAKE BALI NI LA WANANCHI WOTE
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga akizungumza jana wakati akifungua mafunzo yanayohusu usimamizi bora wa shughuli za Halmashauri kwa Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida. Kushoto ni Naibu Meya Jiji la Arusha, Veronica Mwelange.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga
amesema suala la kuleta maendeleo ya nchi sio la Rais Samia Suluhu Hassan peke yake bali ni la wananchi wote.
Dk. Mganga ameyasema hayo jana wakati akifungua
mafunzo yanayohusu usimamizi bora wa shughuli za halmashauri kwa Wenyeviti wa Halamashauri na Mameya yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)
Kampasi ya Singida.
"Suala la kuiletea nchi maendeleo sio la
Rais peke yake bali ni la kila mmoja wetu mahali popote alipo na hii dhana ya
kusema ni jukumu la mkuu wa nchi halina mashiko," alisema Dk. Mganga.
Alisema mafunzo hayo yamekuja wakati sahihi
ambapo taifa letu chini ya Rais Samia linapambana kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kasi.
Dk. Mganga aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo
yamelenga kuwajengea uwezo kwenye maeneo muhimu ya uongozi na utawala bora,
namna ya kubuni vyanzo vipya vya mapato na usimamzi wa makusanyo ya
halmashauri, usimamizi bora wa miradi ya maendeleo kwa kutumia mfumo wa force
account pamoja na upangaji, ufuatiliaji na tathimini ya miradi ya maendeleo.
"Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu wenyeviti
wa halmashauri na mameya kwa kuwa yanalenga kuwaimarisha katika kuhakikisha kuwa
mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo ili kuleta tija na matokeo makubwa.
Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida, Dk. James Mrema akizungumza kwa niaba ya
Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA (CEO), Profesa William Pallangyo alisema wameandaa mafunzo
hayo lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wenyeviti na mameya juu ya namna ya bora
ya kuongoza na kuendesha shughuli za halmashauri hasa kwenye masuala yanayohusu
ukusanyaji wa mapato na mambo mengine.
"Katika mafunzo haya tunategemea wenyeviti
wa halmashauri na mameya waweze kwanza kujua majukumu yao ukizingatia kuwa wao
ndio wasimamizi wakuu katika maeneo yao na kuwa kutakuwa na mada mbalimbali
zitakazotolewa na baada ya mafunzo hayo waweze kurudi katika vituo vyao vya
kazi na kufanyakazi kwa umahiri mkubwa," alisema Dk.Mrema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi , Idrisa Omari Mgaza, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kwani yatawaongezea ujuzi ambao wataenda kuhufanyia kazi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Post a Comment