SUA WAKABIDHIWA HEKTA 10,000 KWAAJILI YA KILIMO CHA MITI NA MAFUNZO MADABA
12-07-2023 MADABA MKATABA.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimesaini Mkataba rasmi na Halmashauri ya Wilaya ya Mdaba Mkoani Ruvuma wa umiliki wa Shamba la Hekta 10,000 kwaajili ya kilimo cha miti na mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wake na jamii.
Akizungumza kabla ya kusaini Mkataba huo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala kwa niaba ya
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la shamba hilo ni kwa ajili ya mafunzo pamoja na kuongeza mapato.
‘’Hivi Sasa Serikali inahimiza vyuo kuongeza mapato yake ya ndani ili viweze kujiendesha badala ya kutegemea ruzuku ya serikali na sisi kama Chuo Kikuu cha Sokoine tumebobea kwenye masula ya misitu na kupitia uzoefu wetu tulioupata kwenye Msitu wetu wa Olmotonyi kule Arusha
tumeona tuje kuwekeza hapa Madaba na tunaamini tutakuwa mfano kwa
vyuo vingine‘’ alieleza Prof. Mwatawala.
Amesema kuwa kasi ya upandaji wa miti kwenye shamba hilo la Ifinga imeongezwa nguvu sasa na Mradi wa HEET ambao umetenga fedha kwajili ya kupanua shamba hilo na kuongeza idadi ya miti itakayopandwa ambapo kwa mwaka huu pekee wanatarajia kupanda hekta 500.
Prof. Mwatawala amesema eneo la shamba walilolichukua baada ya kulipa fidia wananchi kwenye kijiji cha Magingo kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata mazao hayo ya mistu na kuongeza thamani kutaleta maana endapo kiwanda hicho kitapata miti ya kuchakata hasa kutoka kwenye
shama hilo.
Akitoa salamu za Wilaya ya Madaba Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo bwana Sajidu Idrisa amesema anaamini ujio wa SUA sio tu kwamba utasaidia kuchochea kasi ya upandji wa miti lakini pia utasidia kuongeza kipato kwa wananchi watakaoajiriwa kwenye shamba hilo lakini pia vijiji na
Halmashauri.
‘’Ili Halmashauri ifanye vizuri na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo lazima iweze kuwa na mapato ya kutosha kupitia shughuli zake mbalimbali kwahiyo ujio wenu tunaamini Chuo kitapata fedha na kuongeza mapato yake ya ndani lakini pia Halmashauri yetu pia itapata mapato
kutoka kwenu na wawekezaji wengine‘’ Alieleza Bwana Idrisa.
Ametumia nafasi hiyo kuwashauri SUA kuendelea kuongeza kasi ya upandaji wa miti kwenye shamba hilo na kusaidia kufundisha jamii mbinu bora za kilimo cha miti na namna ya kukabiliana na majanga ya moto ambayo yanathiri sana kilimo hicho.
Nae Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima amesema tayari wameshapanda takribani hekta 1000 za miti ya mbao toka mwaka 2018 walipopata eneo hilo na kasi ya upandaji inaongezeka kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
‘’Tumeendelea kuwa na mahusiano mazuri na halmashauri lakini pia wananchi wa kijiji cha Ifinga ambapo katika kipindi hicho Chuo kimefanya mambo mbalimbali kama mchango wake kwa jamii ikiwemo ujenzi wa Matundu 20 ya vyoo kwenye shule ya msingi Ifinga, Kutoa elimu ya moto
kwa jamii pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa kijiji na madiwani‘’ alieleza Dkt. Sirima.
Ameongeza kuwa pamoja na mchango huo lakini pia Shamba hilo linatoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 ambao hufanya kazi mbalimbali za upandaji na huduma zingine za shamba na hivyo kujipatia kipato cha kuendesha familia zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Mhe. Teofawe Mlewa ambaye ameongoza utiaji saini huo kwa niaba ya wananchi amesema kuna mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika kata ya Matumbi baada ya kukaribisha wawekezaji tofauti na hapo awali miaka 7 iliyopita.
‘’Tuna kila sababu za kuwashukuru wawekezaji na uongozi wa Halmashauri ya Madaba kwa kazi kubwa inayofanywa ya kuleta maendeleo kwenye kata ya Matumbi na kijiji cha Ifinga maana sasa toka Dunia iumbwe kuna mabasi aina ya coaster zinafika hadi kijijini kwakuwa barabara ni nzuri
lakini zamani tulikuwa tunatembea kwa miguu kilometa zaidi ya 50 nikiwa
mtendaji‘’ alieleza Mhe. Mlewa.
Amewataka viongozi wa vijiji na kata pamoja na wanachi kuendelea kuwapokea wawekezaji kwenye vijiji vyao kwa kufuata sheria na taratibu ili kuchochea maendeleo badala ya wao kuwa vikwazo na kukwamisha uwekezaji kwenye maeneo yao na kurudisha nyuma maendeleo yao.
Mkataba huo kati ya SUA na Halmashauri ya Wilaya ya Madaba umesainiwa na kushushuhudiwa na viongozi wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Teofawe Mlewa, Diwani wa kata hiyo Mhe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba Mhe. Teofawe Mlewa akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Kijiji cha Ifinga.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala akitoa salamu za SUA kabla ya kusaini Mkataba huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo bwana Sajidu Idrisa akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo.
Viongozi wakiweka saini kwenye mkataba huo.
Picha ya pamoja ya Viongozi wa SUA na Viongozi wawakilishi wa Wilaya ya Madaba wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kusaini Mkataba huo.
Post a Comment