Header Ads

test

VIONGOZI, WATENDAJI WILAYA YA SINGIDA WATAKIWA KUTUMIA MATOKEO YA SENSA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA MAENDELEO

 

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akihutubia wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

...................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

VIONGOZI  na watendaji wa ngazi mbalimbali za utawala katika Wilaya ya Singida na Halmashauri ya Manispaa ya Singida mkoani hapa wametakiwa kutumia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika kufanya maamuzi na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida leo Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

"Mafunzo haya yanatekelezwa kwa mujibu wa Mpango kazi wa Usambazaji na Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa unaotokana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhahiri kuwa si kila mdau tukiwemo miongoni mwetu tunafahamu vyema kutumia matokeo ya Sensa katika kufanya maamuzi na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ambapo Serikali iliona ni vyema kutoa mafunzo haya kwa wadau mbalimbali katika ngazi mbalimbali za kiutawala kuhusu namna ya kutumia matokeo ya Sensa," alisema Mragili.

Alisema mafunzo hayo kwa namna moja au nyingine yatawapa uwezo wa kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu sera na mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kuwa wapo karibu nao, hivyo kutumia matokeo ya Sensa watatekeleza majukumu yao vizuri ya kuwawakilisha wananchi.

Mragili alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Singida kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida na Ofisi ya  Taifa ya Takwimu kwa kuratibu vyema maandalizi ya mafunzo hayo.

Meneja wa Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa alisema mafunzo hayo ni mfufulizo wa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa kwa makundi mbalimbali katika jamii  yanayoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Usambazaji na Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022

"Hadi sasa, mafunzo kama haya yamefanyika kwa makundi mbalimbali yakiwemo viongozi wa ngazi za chini katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Kigoma na Morogoro pamoja na mikoa mitano ya Zanzibar," alisema Kipuyo.

Kipuyo aliyata makundi mengine yaliyopata mafunzo hayo kuwa ni Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa mikoa, Kamati za Sensa za Mikoa na wajumbe wa Sekretarieti ya Mikoa ya Lindi, Mtwara,Pwani,Singida na Wilaya ya Iramba.

Alisema mafunzo mengine yamefanyika katika ngazi ya mkoa katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma. Hivi sasa tunaendelea na mafunzo ya aina hii katika ngazi ya Halmashauri na majiji katika mikoa ya Dar es salaam na Dodoma.

Alitaja kundi jingine lililofaidika na mafunzo hayo kuwa  ni vyombo vya habari ambapo wahariri wa habari wa redio zaidi ya 120 nchini pamoja na wanachama 25 wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Singida na kuwa yataendelea kufanyika kwa ngazi zote za utawala na kuhusisha makundi kama vile viongozi wa siasa, dini, mila na destruri, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu na za kitafiti, Watu Wenye Ulemavu,vyombo vya habari na wananchi wa kawaida.  

Kipuyo alisema  madhumuni ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kuwajengea uwezo wadau wote wa namna ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na utendaji katika Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi ikiwemo biashara na uwekezaji, tafiti, utoaji huduma mbalimbali zikiwemo za kijamii na uchumi.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Serikali, Sekta Binafasi na wananchi kwa ujumla ili kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga alisema kuhusu maelekezo ya Serikali juu ya matumizi ya matokeo ya Sensa, mkoa huo umejipanga kuhakikisha mipango yao  na programu zao zote za maendeleo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022.

"Nieleze kuwa katika mipango na programu zetu za mwaka wa fedha 2023/24 zimezingatia matokeo ya Sensa na Takwimu nyingine zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu," alisema Dk.Mganga.

Alisema mbali ya kutekeleza maelekezo ya Serikali, mkoa umeweka msisitizo wa matumizi ya matokeo ya Sensa kwa lengo la kuhakikisha kuwa mipango na programu hizo zinajibu changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanapambana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Aidha, Dk. Mganga alisema matumizi ya matokeo hayo ya sensa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati na zenye ubora unaozingatia mahitaji halisi kulingana na idadi yao, jinsi yao, kuzingatia mahitaji maalum ya makundi mbalimbali katika jamii na hali ya mazingira wanamoishi.

Alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa sababu yanawajengea uwezo wa kuyatafsiri na kuyatumia matokeo ya Sensa ipasavyo na hatimae kukuza uchumi wa mkoa, kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi na kuchagiza harakati ya kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Meneja wa Takwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, akitoa taarifa za takwimu kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk.Albina Chuwa, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Mkoa wa Singida, Stephen Pankras akiwatambulisha viongozimbalimbali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili wakati wa mafunzo hayo.
Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo
Mbunge wa Singida, Kaskazini, Ramadhan Ighondo, akizungumza kwenye mafunzo hayo ambapo aliomba yapelekwe kwa wananchi waliopo vijijini.
Taswira ya mafunzo hayo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa mafuno hayo
Mtakwimu Mwandamizi, Mdoka Omari, akitoa mada wakati wa mafunzo hayo.


No comments