PROFESA NDALICHAKO AZINDUA MRADI KAZI ZENYE STAHA SEKTA YA PAMBA, SERIKALI KUZIFANYIA KAZI CHANGAMOTO ZA KUITENDAJI
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amesema anafahamu zipo changamoto za kiutendaji ambazo Serikali inaendelea kuzifanyia kazi kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa ya utulivu na amani.
Pia amesema wapo baadhi ya watendaji na watumishi wa idara ambao bado wanalalamikiwa kwa vitendo vinavyokiuka maadili ya Utumishi wa Umma, hivyo ametoa rai kwa watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi
Akizungumza leo Oktoba 21, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Watumishi wa Idara ya Kazi pamoja na Uzinduzi wa Mradi wa Kazi zenye Staha katika sekta ya Pamba Profesa Ndalichako ametumia nafasi kuelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha idara ya kazi.
"Ninaimani kwa mjadala na mada zitakazotolewa mtabadilika na ninaomba kuwaasa kwamba pamoja na kazi nzuri ambayo inafanyika niwakumbushe hatutasita kuwachukulia hatua stahiki watumishi mtakaobainika kujihusisha na ukiukwaji wa Maadili ya Utumishi wa umma yanayoharibu taswira ya Ofisi."
Pamoja na hayo amesema wamepata Mradi wa kukuza kazi za staha katika kilimo cha zao la pamba kwa ufadhili wa Serikali ya Brazil na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambao utetekelezwaji wake utahusisha na usimamizi wa ofisi yao.
"Maofisa Kazi Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa wasimamizi katika Mradi huu ni rai yangu mshirikiane kwa karibu na Wizara na Taasisi zingine zinazohusika katika utekelezaji wa mradi huu ambao kama mnavyofahamu utachukua miezi 24 kuanzia sasa, " amesema Profesa Ndalichako.
Pia amewataka wajitolee na kufanya kazi kwa bidii ili malengo ya mradi huo yaweze kukamilika kwa ufanisi huku akifafanua miongoni mwa masuala yatakayosimamiwa na Ofisi yao ni kuhakikisha watoto hawatumikishwi katika Mkoa wa Simiyu ambao ndio unaongoza kwa kilimo cha pamba na kutumia watoto katika kulima na kuvuna na kukiuka haki za Mtoto ambaye jamii inapaswa kumlinda na viahatarishi vya aina yoyote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)Kanda ya Afrika Mashariki Jealous Chirove amesema mpango huo ni uthibitisho wa ushirikiano wenye manufaa kati ya Shirika hilo na Serikali ya Brazili, unaotekelezwa chini ya Mpango wa Ushirikiano wa Brazil na ILO wa kukuza ushirikiano miongoni mwa nchi zinzoendelea.
Amesema Mpango hup ulioanzishwa mwaka wa 2009, unasisitiza kujitolea kwa Brazili kukuza ushirikiano kati ya mataifa katika kutekeleza ajenda ya kazi zenye staha inayojikita katika kanuni za kuheshimu haki za wafanyakazi.
Pia kukuza fursa za ajira, kupanua hifadhi ya kijamii, na kuendeleza majadiliano mahali pa kazi."Shirika la Kazi Duniani ambalo Tanzania ni Mwanachama, kwa muda mrefu limekuwa mtetezi wa kazi zenye staha, kwa imani kuwa ajira ni utu, tija, na chombo cha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa jumla.
"Tanzania, kama yalivyo mataifa mengine mengi, inakabiliwa na changamoto ya kutokomeza utumikishwaji wa watoto. Sekta ya pamba, ambayo ni sekta muhimu ya uchumi wa Tanzania, haijaachwa na changamoto hii.
"Tumekutana kuzindua mradi unaoashiria azimio letu la pamoja la kuvunja mzunguko huu wa utumikishwaji wa watoto, umaskini na ukosefu wa usawa. Malengo yetu ni pamoja na kuimarisha hifadhi ya kijamii kwa wafanyakazi katika sekta ya pamba," amesema Chirove.
Mengine ni kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa kupambana na utumikishwaji wa watoto na kuimarisha ulinzi wa watoto katika ngazi za Serikali za mitaa, kuongeza uelewa kuhusu utumikishwaji wa watoto katika mikoa inayolima pamba, na kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa kazi, inayozingatia kutokomeza utumikishwaji wa watoto.
Amesema juhudi hizo hizi zinatarajiwa kuboresha maisha ya watoto kwa kuwapa fursa za elimu bora na kulinda haki zao, kuwa minyororo endelevu ya pamba na yenye kuwajibika kwa jamii, kwa kutangeneza fursa za ajira zenye staha na kuchangia maendeleo ya jamii.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani(ILO) Kanda ya Afrika Mashariki Jealous Chirove akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Post a Comment