Header Ads

test

TMA YATANGAZA UWEPO WA MVUA NYINGI KWA MAENEO YANAYOPATA MSIMU MMOJA WA MVUA KWA MWAKA

Na Karama Kenyunko Michuzi tv 


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha uwepo wa mvua nyingi katika kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu wa Novemba, 2023  hadi Januari, 2024 na kwamba zinaweza kusababisha mafuriko na kuathiri ukuaji wa mazao.

Imesema uwepo wa El-NiƱo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu huo ikilinganishwa na kipindi cha nusu ya pili cha  Februari hadi Aprili, mwaka 2024.

Akitangaza uelekeo wa mvua hizo leo Okroba 31, 2023 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dkt Ladislaus Chang’a, ameyataja maeneo yatakayopata mvua za juu ya wastani kuwa ni Kusini mwa Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. 

Aidha, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa Kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma.

Dkt Chang'a amesema katika mvua hizo,  athari zitakazojitokeza ni pamoja na vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.

Vilevile amesema magonjwa kama vile ukungu yanatajariwa kuongezeka na kuathiri mazao kama viazi mviringo, nyanya, ufuta na maharage. 

"Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika maeneo mengi hata hivyo, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hivyo wadau mbalimbali wanashauriwa kuzingatia matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali maji," amesema.

Pia amewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba, na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huo.

Aidha, imeshauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo pamoja na uvunaji maji ya mvua na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

"Huu ni uelekeo wa mvua za msimu Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni mikoa ya  Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na  na Kusini mwa Morogoro," amesisitiza.

Ameeleza kuwa mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo ya Magharibi na kutawanyika katika maeneo mengine mwezi Novemba, 2023.

Amefafanua kuwa msimu wa vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Desemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, mvua hizo zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu Kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa.

"Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) utabiri wake ulitolewa tarehe 24 Agosti, 2023," amesisitiza.

Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023, vilevile, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka  leo Oktoba 31, 2023 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka  leo Oktoba 31, 2023 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni mkurugenzi Huduma za Utabiri - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa na kulia ni Dkt. Alfred Kondowe.

No comments