Header Ads

test

WAZIRI SIMBACHAWENE AZINDUA MWONGOZO WA UJUMUISHWAJI JINSIA KATIKA UTUMISHI WA UMMA, AWAPONGEZA UONGOZI INSTITUTE

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene ametoa rai kwa waajri wote kutumia kikamilifu Mwongozo wa ujumuishwaji wa jinsia katika utumishi wa umma kuwaelimisha watumishi na wadau kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika shughuli za kila siku katika utumishi.

Ametoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa ujumuishwaji wa jinsia katika utumishi wa umma pamoja na ufunguzi wa Mafunzo ya Wanawake awamu ya tatu na nne yaliyoandaliwa na Uongozi Institute.

“Baada ya kuzinduliwa kwa mwongozo huu ni matarajio yangu kuona mwitikio mkubwa wa Waajiri wote Tanzania Bara kwenye kutekeleza na kutenga bajeti kila mwaka wa fedha ili kumuwezesha Mratibu wa masuala ya Jinsia wa Taasisi husika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na uratibu wa mafunzo ya Jinsia katika Utumishi wa Umma kwenye Taasisi husika,”amesema.

Aidha ametoa maelekezo kdhaa ya kuwezesha kuufanikisha mwongozo huo  yakiwemo Waajiri wote katika Utumishi wa Umma kuuelewa vyema na kuutekeleza Mwongozo wa ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma.

Pia Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ihakikishe inasambaza Mwongozo wa ujumuishwaji wa Jinsia katika Taasisi zote za Umma Tanzania Bara.

Mengine ni Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ishirikiane na TAMISEMI kuzifikia Mamlaka zote katika Mikoa 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 ili kutoa mafunzo kuhusu Mwongozo huo  ili kila mtumishi wa umma apate uelewa wa kutosha.

“Mamlaka zote za Ajira Tanzania Bara ziandae Mpango kazi wa namna ya kutekeleza Afua za usimamizi wa masuala ya Jinsia Mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma kama ilivyoainishwa katika Mwongozo.

“Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ishirikiane na Mamlaka zote za Ajira kuendesha mafunzo kuhusu mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma ili kuimarisha usawa na hatimaye kuondoa aina zote za ubaguzi mahali Pa Kazi.”

Pia ameipongeza Taasisi ya UONGOZI kwa kuendelea kubeba jukumu hilo la kuwajengea uwezo viongozi wanawake kwenye masuala ya uongozi lakni pia kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha usawa wa kijinsia katika mambo mbalimbali ikiwepo hili la uongozi.

 “Leo hii pia tunawapongeza viongozi waliopata nafasi ya kipekee kushiriki kwenye programu hii ya mafunzo ya uongozi kwa wanawake inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI.Nimefahamishwa kuwa programu hii maalumu inalenga kutoa mafunzo kwa viongozi wa juu …

“Na wanaochipukia  ili kuongeza na kukuza sifa za uongozi kwa wanawake, kuchanganua changamoto zinazowakwamisha katika kufikia ngazi za juu zaidi, kutambua changamoto za kijinsia zenye kuathiri mafanikio yao na kuboresha tabia na mienendo binafsi itakayowawezesha kufanikiwa katika safari za uongozi.”

Ametoa rai kwa wanufaika kwa programu hiyo wakimaliza mafunzo hayo, watakuwa mabalozi wazuri wa program hiyo kwa kubadilishana maarifa na ujuzi walioupata na viongozi wengine na hasa wale viongozi chipukizi.

“Ili kwa pamoja tuweze kufikia usawa wa kijinsia nchini, hasa  kweye mausala ya uongozi, hatuna budi kushirikisha wanaume katika utekelezaji wa mipango na jitihada mbalimbali za kufanikisha azma za wanawake kuwa viongozi,”amesema Waziri Simbachawene

Amependekeza Taasisi ya UONGOZI kuendelea kuwashirikisha na kuwahusisha kikamilifu wanaume kwenye hii programu ili kuleta matokeo yenye tija huku akitumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa  washirika wao wakubwa ambao ni Serikali ya Finland na Umoja wa Ulaya (EU).

Wengine ni  Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN WOMEN) kwa kuendelea kusaidia Taasisi kifedha na ki-utaalamu katika kutimiza majukumu yake kuwajengea uwezo viongozi hususan wanawake.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu  wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo ameeleza kwamba maombi ya washiriki waliomba awamu ya nne  walikuwa watu 800 kutoka maeneo mbalimbali ambapo Chuo kimechukua watu 100.

Amefafanua kati ya washiriki 100 kati yao wameweza kuchukua washiriki wachache kutoka nchi za nje ambapo watashiriki mafunzo hayo.

"Mafunzo haya yapo katika ngazi tatu ikiwemo jukwaa la uongozi wa wanawake, mafunzo pamoja  na kuwasimamia na kutoa ushauri katika mafunzo wanayopata ya uongozi, " amesema.
Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Menejimenti ya Umma na Utawala Bora George Simbachawene (katikati) Akizindua Mwongozo wa ujumuishaji wa jinsia katika utumishi wa umma.







Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Menejimenti ya Umma na Utawala Bora George Simbachawene (katikati) Akizindua Mwongozo wa ujumuishaji wa jinsia katika utumishi wa umma.



Matukio mbalimbali katika picha wakati wa uzinduzi ws Mwongozo wa ujumuishwaji wa jinsia katika utumishi wa umma pamoja na ufunzi wa mafunzo ya Awamu ya Tatu na Nne kwa wanawake viongozi.

No comments