WIZARA YA AFYA YAWASILISHA MAPENDEKEZO YA KUANZISHWA KWA TAASISI YA DAWA AFRIKA
Wizara ya Afya leo Tarehe 17/10/2023 imewasilisha mapendekezo kuhusu azimio la kuridhia Mkataba wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Dawa ya Afrika (Treaty for the Establishment of the African Medicines Agency AMA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala UKIMWI inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Stanslaus Nyongo.
Akiwasilisha taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema kuwa Taasisi hiyo itasaidia kuratibu na kusaidia nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kuboresha uwezo wa kudhibiti ubora wa bidhaa tiba hususan katika maeneo ambayo ni changamoto kwa nchi nyingi barani Afrika.
“Taasisi hii itaisaidia Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) kutatua changamoto mbalimbali katika udhibiti wa bidhaa tiba ikiwemo upungufu wa wataalamu, uwepo wa njia zisizo rasmi katika maeneo ya mipaka na vituo vya forodha visivyoruhusiwa kuingiza bidhaa tiba” amesema Dkt. Jingu.
Amesema changamoto nyingine ni mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia yanayohitaji mbinu mpya na weledi maalumu katika kudhibiti bidhaa tiba, hali ambayo inahatarisha afya ya jamii kwa kuwa bidhaa tiba duni na bandia zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zinaendelea kuwepo katika soko.
Katika kutekeleza jitihada za pamoja za kutatua changamoto hizo, Wakuu wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Umoja wa Afrika katika mkutano wa kawaida wa 32 (Assembly/AU/Dec. 735(XXXII) uliofanyika Addis Ababa Ethiopia tarehe 11 Februari, 2019, walikubaliana kuanzishwa kwa Taasisi ya Dawa ya Afrika (African Medicines Agency – AMA)
“Ili taasisi hiyo ianze kufanya kazi, nchi wanachama zinatakiwa kusaini na kuridhia Mkataba huo na hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2023 jumla ya nchi 30 zimesaini na kati ya hizo 23 zimeridhia Mkataba wa AMA huku Tanzania imesaini Mkataba huo tarehe 10 Agosti, 2021 na hatua inayofuata ni kuridhia ili kujiunga na Taasisi hiyo” amesema Dkt. Jingu.
Post a Comment