Header Ads

test

MKOA WA RUVUMA KUANZA BIASHARA YA HEWA UKAA

 


Wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma zimeingia mkataba wa
biashara ya hewa ukaa (Carbon) na  Kampuni ya Tanzania Carbon(CT
Limited) kutoka mkoani Arusha.

Mkataba wa kuanza biashara hiyo umesainiwa kwenye ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma mjini Songea chini ya Usimamizi wa Katibu Tawala wa
Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki ambaye alimwakilisha Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.

Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo,Mkurugenzi wa Kampuni ya
CT Limited Marc Backer amelitaja lengo la Kampuni ya Carbon Tanzania
kuwa ni kuhakikisha wananchi wanafaidika kiuchumi na kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti.

Amesema hapa nchini wananchi wa vijiji nane katika Halmashauri ya
wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wameingiza zaidi ya bilioni 2.3 kwa
kufanya biashara ya hewa ya ukaa.

“Mradi huu umewanufaisha wananchi wa wilaya za Tanganyika mkoani
Katavi na Kiteto mkoani Manyara,hapa Ruvuma mradi wa biashara ya
kaboni utakuwa mkubwa sana,tumeshapima tumegundua kuna kaboni
nyingi sana’’,alisisitiza Backer.

Backer amesema biashara ya hewa ya ukaa ilianza rasmi mwaka 2018
katika Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi kwa kuendeshwa na
Taasisi ya Carbon Tanzania ambapo mapato ya biashara hiyo yamekuwa
yakipanda mwaka hadi mwaka.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro
ameitaja mikataba ya biashara ya kaboni kuwa ina faida kubwa hata kama
msitu utatunzwa kwa miaka 60 unaleta faida kwa wananchi wenye misitu
ikiwa ni Pamoja na kuleta mvua nyingi na kwamba wananchi watapata
fedha nyingi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya
amesema biashara ya hewa ukaa ni mradi mpya hapa nchini na kwamba
baada ya majaribio katika wilaya ya Tanganyika serikali imeona faida
kubwa.
Amesema biashara hiyo inamwezesha mwananchi kupata fedha baada ya
kupanda miti ambapo ameitaja wilaya ya Namtumbo kuwa ni wilaya ya

kimkakati kwa kuwa asilimia 19 ya maji yanayoingia kwenye mradi wa
bwawa la Mwalimu Nyerere Rufiji yanatoka Namtumbo.

Amesisitiza kuwa biashara ya hewa ukaa ni mradi ambao utasaidia
kutunza mazingira na kuhakikisha kuwa uharibifu wa mazingira unakwisha
na kwamba mradi utaleta mvua za kutosha na dhana ya Mkoa wa Ruvuma
kuwa ghala la Taifa la chakula itaendelea kuwepo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki amewaasa
wakulima kuhakikisha wananufaika na mradi wa kaboni kwa kuhakikisha
wanapanda miti ya kutosha badala ya kuishia kulima mahindi na mazao
mengine.
Amewaasa wakulima kupanda miti kwa wingi na kuhifadhi misitu ili
kupunguza hewa ya ukaa na kuongeza upatikanaji wa hewa safi lakini pia
watakuwa wanafanya biashara ya hewa ya ukaa.

Tanzania imesaini mikataba ya Kimataifa ambayo inahamasisha biashara
ya hewa ya ukaa Duniani ambapo wananchi wanapopanda miti na
kuhifadhi misitu inasaidia kufyonza na kupunguza hewa ya ukaa hewani
na kulipwa fedha hivyo kukuza uchumi wao.

Soko la hewa Safi ya Kaboni  lililopo ni fursa muhimu kwani Dunia
imedhamiria kuboresha Anga kutokana na madhara ya uharibifu wa hewa
chafu ya kabon  ili kuokoa anga na ongezeko la Joto duniani.


 wWakuu wa wilaya za Namtumbo mheshimiwa Ngollo Malenya na Mkuu wa  wialya ya Tunduru mheshimiwa Julius Mtatiro wakiwa na wakurugenzi wa Halmashauri hizo wakiwa kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa biashara ya hewa ukaa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,zoezi hilo lilishuhudiwa na Katibu Tawala wa wa Mkoa wa Ruvuma ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Carbon Limited kutoka mkoani Arusha Marc Backer akiweka saini moja ya mikataba kutoka wilaya za Namtumbo na Tunduru.
 i Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzania Carbon Limited kutoka mkoani Arusha Marc Backer akizungumza kwenye hafla ya kuweka saini mkataba wa biashara ya hewa ukaa (Carbon) baina ya Kampuni hiyo na wawakilishi kutoka wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma,Hafla hiyo imefanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
Wawakilishi kutoka wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa na Kampuni ya Tanzania Carbon wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika zoezi la utiaji saini mkataba wa biashara ya hewa ukaa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.

No comments