Header Ads

test

Huduma ya Bima itakayotolewa Airtel kwa kushirikiana na Jubilee Insurance pamoja na Axieva itaenda kuokoa maisha na uchumi wa watanzania-Waziri Nape

 

 

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Technolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amezipongeza kampuni ya Airtel Tanzania kwa ushirikiano wake na kampuni za Jubilee Insurance pamoja na Axieva kwa kuanzisha huduma Afya Bima, akisema huduma hiyo imekuja wakati muafaka katika kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan akisaini muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwapa fursa watanzania wengi zaidi kunufaika na mpango huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, wakati akitambulishwa rasmi huduma hiyo, Waziri Nape alisema, huduma ya Afya Bima itakayotolewa Airtel kwa kushirikiana na Jubilee Insurance pamoja na Axieva itaenda kuokoa maisha na uchumi wa watanzania wengi ambao hawakuwa katika mfumo wa bima ya afya hivyo kulazimika kutumia pesa taslimu na wakati mwingine kulazimika kuuza rasilimali zao ili kujitibu wao ama wategemezi wao.

“Nichukue nafasi hii kuzipongeza Airtel Tanzania, Jubilee Insurance pamoja Axieva kwani huduma hii inapatikana kirahisi kwa njia ya kidigitali kupitia Airtel Money hivyo kuwafanya watanzania wengi zaidi kujiunga mahali popote walipo bila usumbufu.

“Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika kuongeza miundo mbinu mingi ya kutoa huduma za afya, ujenzi wa zahanati katika ngazi ya vijiji, vituo vya afya katika ngazi ya kata, hospital za halmashauri , hospital za rufaa za mikoa, hospital za Kanda pamoja na hospital za kitaifa hivyo ujio wa Afya Bima utasaidia watanzania wengi kuweza kunufaika na huduma bora za afya zitolewazo katika hospitali za umma”, alisema Waziri Nape.

Waziri Nape aliongeza kuwa uwekezaji wa Serikali katika kutengeneza miundombinu ya afya hautakuwa na maana kama wananchi watakuwa wanapata huduma hizo kwa kusuasua na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita ikaamua kusukuma ajenda ya Bima ya afya kwa wote.

“Jambo kubwa ni kwamba Bima hii, imewalenga watanzani wote hasa ambao hawana uwezo wa kuweza kujigharamia matibabu pindi wakipata shida ya kuumwa kama madereva bodaboda na Mama ntilie kwa hiyo jambo hili ni suluhisho kubwa kwao kupata huduma za afya huku Maisha yao yakiendelea”, Alisema Waziri Nape.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Airtel Money, Bwana Charles Rugambwa alisema huduma ya Afya Bima ni moja ya mikakati ya Airtel katika kuwaletea watanzania huduma bora za kiubunifu na rahisi kujiunga kwa njia ya kidigitali ambapo wateja wote wa Airtel Money wanaweza kujiunga kwa kutumia simu janja na ya kawaida.

“Kwa kuwa huduma ya Afya Bima ni kwa ajili ya watu wote na hiki ni kipindi cha msimu wa sikukuu za kuelekea mwaka mpya, natoa wito kwa wateja wa Airtel Money kuwapa zawadi wapendwa wao kwa kuwalipia vifurushi ya Afya Bima, hii ni zawadi ya ukweli.

“Ni rahisi kujiunga, mteja wa anachotakiwa kufanya ni kuingia katika menu ya Airtel Money kisha anaingia namba 6, Huduma za kifedha, kisha 2, Bima, kisha 2 tena, Afya Bima, kisha kuthibitisha na baadae kuchagua aina ya vifurushi ukitakacho”, alisema Bwana Rugambwa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Jubilee, Dk. Harold Adamson amesema kuwa wamefarijika kuwapata wadau ambao wameshirikiana nao katika kuongeza thamani ya tehama na kuhudumia moja kwa moja kwenye Maisha ya watanzania wote.

“Sisi kama Jubilee tumefarijika kuweza kupata wadau wenzetu ili kuanzisha huduma na bidhaa hii mpya kwa watanzania hasa wanaotumia mtandao wa airtel, bidhaa hii ya afya bima inaunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na bima ya afya”, Alisema Dkt. Adamson.

Akitaja baadhi ya manufaa na Afya Bima, Dk. Adamson alisema, Afya Bima inakuja na bima za afya aina tatu ambazo ni Afya Poa, Afya Supa na Afya Dhahabu ambapo mteja ataweza kuchagua vifurushi tofauti kulingana na uhitaji wake.

“Bima ya Afya Poa inalenga kurudisha mapato yaliyopotea wakati mgonjwa alipolazwa ambapo mgonjwa anapokuwa amelazwa atakuwa anarudishiwa gharama kati ya Tzs 20,000 mpaka Tzs 50, 000, vile vile, Afya Poa inatoa faida ya bima ya gharama za mazishi ya mpaka Tzs 1 milioni moja, ajali, ulemavu au kifo faida ya mpaka Tzs 500,000 na vifurushi vyake gharama yake kati ya Tzs 6,000, Tzs 7,000 mpaka Tzs 35, 0000 kulingana na uhitahitaji wake.

“Kwa upande Afya Supa na Afya Dhahabu zinatoa faida kwa mteja kupata huduma za matibabu bila malipo, Afya Supa inampa mteja kupata gharama ya matibabu ya hadi Tzs 5 milioni na hii ni pamoja na mteja aliyelazwa au kupata matibabu ya bila kulazwa. Bima hii ina kufurushi cha kulipia kati ya Tzs 15,000 mpaka Tzs 45,000 kwa mwaka kulingana na mahitaji ya mteja, lakini pia Afya Supa inakuja na faida ya uzazi ya gharama ya hadi Tzs 2 milioni”, alisema.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano amesema kuwa kampuni hiyo inatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya kuhakikisha watoa huduma kupitia Tehama wanatumia ujuzi huo kuwasaidia wananchi wa aina zote na kuipa thamani sekta hiyo.

Alisema kuwa Huduma na Bidhaa mpya ya Afya Bima itakwenda kwa watanzania wapatao milioni 17.5 wanaotumia mtandao huo kuweza kupata matibabu kwa bei nafuu katika vituo zaidi ya 600 nchini na kuwawezesha wananchi kuwa na unafuu wakati wa shida ya kuumwa na kusimama kufanya kazi.

Mteja anayejiunga na Afya Bima ataweza kupata huduma ya matibabu kulingana na hospitali ambazo Wizara ya Afya Imesajili ambazo ni Hospitali za Umma, hospitali za kibinafsi na za Misheni kulingana na orodha iliyotolewa.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu huduma mpya ya Afya Bima inayotolewa na Airtel Money kwa ushirikiano na makampuni ya Jubilee Insurance na Axieva. Waziri Nape alisema Afya Bima itasaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi kiafya na kiuchumi. Wengine ni viongozi kutoka makampuni hayo.
Mkurugenzi wa Airtel Money, Bwana Charles Rugambwa (kulia), akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam leokuhusu huduma ya Afya Bima inayopatikana kwa wateja wote wa Airtel Money wenye simu janja na za kawaida.. Kulia kwake ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Mkurugenzi Mtendaji wa  Jubilee Insurance, Dk. Harold Adamson.

Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano (kushoto), akizungumzia faida mbalimbali watakazozipata wateja wa Airtel Money kwa kujiunga na huduma mpya ya Afya Bima wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini jijini Dar es Salaam leo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Axieva, Davrav Dhingra, akizungumza katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam leo. Kulia kwakwe ni Mkurugenzi wa Airtel Money, Bwana Charles Rugambwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye.

No comments