MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATAKIWA KUHAMASISHA MAMA MJAMZITO KUWAHI KATIKA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA
Madaktari wa Bingwa wa Rais Samia wametakiwa kutoa hamasa kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa na utamaduni wa mama mjamzito kuwahi kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mapema kwa ajili ya kuanza kliniki, kupima afya mara kwa mara ili kujua hali za afya zao na watoto walio tumbloni.
Wito huo umetolewa leo Oktoba, 7, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko wakati akizindua kambi ya Madaktari Bingwa wa Samia watakao toa huduma za kibingwa na bingwa bobezi katika Hospitali tano za mkoa huo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo katika hospitali hizo.
Amesema kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia itasaidia wakazi wa mkoa wa Katavi kujua hali za afya zao kwani wanakatavi ni sehemu ya nguvu kazi ya taifa katika kuleta maendeleo nchini.
“Hivyo nendeni mkatoe hamasa kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya zao kabla ya kuugua ili kujua hali za afya zao na kupata matibabu sahihi kabla ya tatizo kuwa kubwa na kuleta athari kubwa wakati wa matibabu”. Amesisitiza Mhe. Mrindoko.
Lakini pia ameongeza kuwa hamasa nyingine na muhimu sana ni kuhamasisha mama mjamzito kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mapema kwaajili ya kuanza kliniki kwa wakati na kuepuka baadhi ya matatizo yanayoweza kutokea wakati wa ujauzito.
Aidha, amesisitiza hamasa ya wananchi kupata lishe bora na sahihi kwa watoto wadogo, vijana, rika la kati na wazee ambapo amesema lishe sahihi ni mlo wenye virutubisho sahihi ambavyo haviwezi kuharibu afya ya mtu na hiyo ni kulingana na maelekezo ya wataalamu wa lishe katika maeneo yao wanavyoelekeza wakati wa mlo.
Ameendelea kusema kuwa hamasa hiyo itasaidia wananchi kujitambua mapema hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuanza uchunguzi mapema na baadae kuanza matibabu mapepa kabla ya tatizo halijawa kubwa.
“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Katavi namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliofanya katika sekta ya afya hasa kwa kuona umuhimu wa kusogeza Huduma za kibingwa na bingwa bobezi karibu na wananchi na kuleta tija ya kutotumia gharama kubwa kufuata Huduma hizo nje ya mkoa”. Ameshukuru Mhe. Mrindoko.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt. Jonathan Budenu amesema kuwa kambi hiyo ya Madaktari bingwa itatoa huduama za kibingwa kwa siku saba na kutoa ujuzi kwa wataalamu wa afya walipo katika hospitali tano ambazo mabingwa hao watakwenda kutoa Huduma katika mkoa huo.
“Ujio wa madaktari bingwa ni faraja kwa wakazi wa Katavi kwani asilimia kubwa rufaa za nje ya Mkoa zitapungua kwa kiasi kikubwa na kufanya jamii kutotumia gharama kubwa kufuata huduma hizo kwani Rais Samia hizi huduma kazisogeza katika ngazi ya msingi”. Amesema Dkt. Budenu.
Post a Comment