Header Ads

test

MIRADI YA KIMKAKATI KATIKA SEKTA YA UJENZI KUIFUNGUA BAGAMOYO KIUTALII -BASHUNGWA

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo Oktoba 10, 2024

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka msisitizo katika kufungua uchumi wa mji wa kitalii wa Bagamoyo kwa kuboresha miundombinu ya barabara, ikiwemo ujio wa mradi wa barabara ya mabasi ya mwendo kasi kutoka Maktaba, Dar es Salaam.

Aidha, Serikali imeahidi kumalizia kipande cha kilomita 2 cha barabara ya Nianjema, ambacho hakijakamilika kwa kiwango cha lami.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akiwa katika ziara yake maalum kwenye Halmashauri ya Bagamoyo oktoba 9,2024 alieleza ,Serikali inaendelea kutatua changamoto za ujenzi wa miundombinu hatua kwa hatua ili kuboresha usafiri wa barabara na majini wilayani humo.

Alifafanua kuwa ,mabasi ya mwendo kasi yatakwenda hadi Bagamoyo, ambapo mkandarasi ameanza kazi kuanzia Maktaba, Dar es Salaam kupitia Morocco, Kijitonyama, Mwenge,  kuelekea Tegeta, Boko hadi BasiHaya, eneo ambalo limekuwa likisumbua wakati wa mvua kutokana na kukatika kwa barabara.

"Usanifu unaendelea katika eneo hilo, na tunatarajia kuondoa kabisa kero hiyo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo," alisema Bashungwa. "Tunatekeleza mpango huu hatua kwa hatua, tukitambua kuwa Bagamoyo sasa imeunganishwa na Dar es Salaam, hivyo ni muhimu miundombinu iwe ya kisasa na yenye ufanisi."

Vilevile, Waziri Bashungwa alibainisha ,Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inaangalia fursa ya kuunganisha Bagamoyo na Zanzibar kupitia njia ya maji, hatua ambayo itainua zaidi sekta ya utalii.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Makofia-Mlandizi, Waziri Bashungwa alieleza kuwa barabara hiyo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia SGR kuelekea Mlandizi hadi Bagamoyo.

Akizungumzia daraja la Mbweni-Mpiji upande wa Kata ya Mapinga, Bagamoyo, Bashungwa alieleza kuwa usanifu mpya unafanywa baada ya kubainika kuwa mto umepanuka, hivyo kujengwa daraja imara zaidi ili kuepuka hatari ya kusombwa.

"Serikali yenu ni sikivu, na tunafanya kila juhudi kutatua changamoto kulingana na bajeti. Bagamoyo ya kesho itakuwa ya neema," alisisitiza Bashungwa.

Akitoa taarifa ya Barabara ya mita 780 kata ya Nianjema kwa kiwango cha lami, Meneja TARURA Bagamoyo, mhandisi Angetile Bupe, alisema barabara hii ni sehemu ya ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, ujenzi huo umefanyika kuanzia 2021-2022 hadi 2024-2025, ukisimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani.

Bupe aliomba, Serikali iongeze fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 2, kwani ujenzi unafanywa kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha.




 

No comments