Header Ads

test

TRA NA TAFFA ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA USIMAMIZI WA MAADILI YA WATUMISHI

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Shaibu Mmari, amesema ushirikiano kati ya TRA na mawakala wa forodha ni nguzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa maadili na uwajibikaji kwa watumishi wa Mamlaka.

Bw. Mmari amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mazungumzo kati ya TRA na viongozi wa Chama cha Waondoshaji na Wapelekaji Shehena Bandarini na Mipakani Tanzania (TAFFA), kilicholenga kuimarisha mahusiano ya kikazi na kubadilishana taarifa kuhusu uvunjifu wa maadili unaoweza kujitokeza katika shughuli za forodha.

Amesema kuwa ushirikiano wa karibu kati ya TRA na wadau wa sekta ya forodha ni muhimu katika kusaidia kubaini na kudhibiti vitendo vinavyokiuka maadili, pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

“TRA ina jukumu la kukusanya mapato ya Serikali, kusimamia shughuli za forodha, na kuhakikisha sheria na taratibu za ushuru zinafuatwa ipasavyo. Ushirikiano na wadau kama TAFFA unatusaidia kuimarisha uadilifu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu haya,” amesema Bw. Mmari.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wadau kuendelea kushirikiana na TRA katika kutoa taarifa pale wanapoona dalili za uvunjifu wa maadili au vitendo vinavyoweza kuathiri uadilifu wa huduma za forodha.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa TAFFA, Bw. Anthony Mukyamuzi, ameipongeza TRA kwa juhudi inazoendelea kufanya katika kuboresha mifumo ya forodha na utoaji wa huduma kwa wadau.

Amesema maboresho hayo yameongeza ufanisi katika shughuli za uondoshaji na uingizaji wa mizigo bandarini na mipakani, na kuimarisha mazingira ya biashara kwa wadau wa sekta ya usafirishaji na uondoshaji shehena.

Mwisho, pande hizo mbili zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana taarifa, kuhamasisha maadili mema kwa watumishi, na kujenga mfumo wa uwajibikaji utakaosaidia kulinda uadilifu wa shughuli za forodha nchini.

 

No comments