Wadau wa Tiba Asilia wakutana Dodoma kujadili mustakabali wa Sekta
Na Mwandishi Wetu
Dodoma — Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania limetangaza kushiriki rasmi mkutano wa wadau wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala unaoandaliwa na Wizara ya Afya Tanzania, utakaofanyika Machi 25, 2026 katika Mji wa Serikali Mtumba, wilayani Chamwino, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa shirika hilo, Simba A. Simba, mkutano huo unachukuliwa kuwa fursa ya kihistoria kwa wadau wa sekta ya tiba asilia kukutana, kubadilishana mawazo na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuimarisha sekta hiyo nchini.
Amesema kuwa mkutano huo ni hatua muhimu katika kujenga mustakabali wa Tiba Asilia kwa kuzingatia misingi ya ubora, uwajibikaji, heshima na utambuzi wa kitaifa na kimataifa.
“Tiba Asilia haiwezi kutenganishwa na mazingira, kwani rasilimali zake zinatokana na bioanuwai ya nchi. Hivyo, ulinzi wa mazingira ni msingi wa uendelevu wa sekta hii,” alisema Simba.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira vinaathiri moja kwa moja upatikanaji wa dawa asilia, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hizo.
Aidha, shirika hilo limeeleza kuwa katika dunia ya sasa yenye changamoto za magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, Tiba Asilia ina nafasi muhimu ya kuwa sehemu ya suluhisho endapo itaendelezwa kisayansi na kusimamiwa kwa weledi.
Katika mkutano huo, wadau wanatarajiwa kujadili pia namna ya kuunganisha maarifa ya jadi na sayansi ya kisasa, pamoja na kutumia teknolojia mpya ikiwemo Akili Unde (AI) katika utafiti na uhifadhi wa tiba asilia.
Shirika hilo pia limehimiza umuhimu wa ushirikishwaji mpana wa wadau wote, wakiwemo serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu na mashirika ya kijamii, ili kujenga mfumo imara wa kitaasisi utakaoongeza uwajibikaji na ufanisi wa sekta hiyo.
Sambamba na hilo, limependekeza kuimarishwa kwa ujumuishaji wa Tiba Asilia katika mifumo rasmi ya afya, ikiwemo kuingizwa kwenye Bima ya Afya, upatikanaji wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (TMSD), pamoja na kuongeza uwekezaji katika tafiti na ubunifu.
Aidha, shirika hilo limebainisha kuwa Tiba Asilia ina uwezo mkubwa wa kuchangia uchumi wa taifa kupitia ajira na mapato, hivyo kuna haja ya kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na upatikanaji wa mitaji kwa wadau wa sekta hiyo.
Kwa upande mwingine, wadau wamehimizwa kutumia mkutano huo kujenga umoja, kuondoa tofauti zisizo za msingi na kupambana na vitendo vinavyochafua taswira ya sekta, ikiwemo ulaghai na huduma zisizo na weledi.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuweka dira mpya ya maendeleo ya Tiba Asilia nchini, huku wadau wakihimizwa kushiriki kikamilifu kwa manufaa ya taifa.
Huu ni wakati wa kuunganisha nguvu, hekima na uzoefu wetu kwa manufaa ya taifa letu. Muda ni sasa. Tunawahimiza wadau wote kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu muhimu.Imetolewa na: Simba A. Simba Mwenyekiti Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania
Tarehe: 24 Machi 2026
Post a Comment