Header Ads

test

BAOBAB WAKUTANA NA NBAA, WAPATIWA ELIMU YA UHASIBU


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kuimarisha juhudi zake za kutoa elimu kwa wanafunzi mbalimbali wa Sekondari na Elimu ya Juu nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza Taaluma ya Uhasibu na kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Bodi hiyo.

Katika mwendelezo wa juhudi hizo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Baobab wametembelea NBAA na kupatiwa mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uelewa mpana kuhusu shughuli za Bodi pamoja na fursa zilizopo katika Taaluma ya Uhasibu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi , aliipongeza shule hiyo kwa jitihada za kuwawezesha wanafunzi wake kupata elimu ya vitendo nje ya darasa, hususan wale wanaosoma masomo ya biashara na Uhasibu.


Aidha, alieleza kuwa NBAA iko wazi kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu, na aliwasisitiza wasibadilishe taaluma kwa kuwa tayari wana msingi mzuri wa uhasibu. Pia alielezea kuwa hata wanafunzi wa michepuo wa masomo mengine ambao hawajasomea Uhasibu wanaweza kujiunga na mitihani ya Bodi hiyo kuanzia ngazi ya awali na hatimaye kufikia sifa za kuwa wahasibu kitaaluma.

CPA Prof. Siasa I. Mzenzi aliwasisitiza wanafunzi hao kufanya vizuri katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea, alieleza kwamba Taaluma ya Uhasibu ina nafasi kubwa katika Taasisi mbalimbali kutokana na uhaba wa Wahasibu nchini.

Pia aliongeza kwa kuanzia ngazi za awali za masomo kunawasaidia wanafunzi kujengwa kitaaluma na kuwa wahasibu bora wa baadaye, huku akisisitiza umuhimu wa uadilifu, uaminifu na kufanya kazi kwa bidii bila kusimamiwa ili kuendeleza na kulinda hadhi ya Taaluma hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi hao, kwani imewapa fursa ya kupata taarifa sahihi na muhimu kuhusu majukumu ya Bodi pamoja na mwelekeo wa Taaluma ya Uhasibu.

Naye mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Baobab, Stephen Mahundi, aliishukuru NBAA kwa kuwapatia wanafunzi elimu ya Uhasibu, akisema itawasaidia katika masomo yao ya sasa na kuwaandaa kufikia malengo yao.

Ziara hiyo ni miongoni mwa juhudi za NBAA za kuendelea kujenga kizazi cha wataalamu wa Uhasibu wenye uelewa mpana na uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa na kukuza uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Tano wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Baobab waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA zilizopo jijini Dar es Salaam.
CPA. Bertha Kipangula, Mkuu wa Sehemu ya Usajili wa Wanachama, Uzingatiaji wa Sheria na Maendeleo ya Kitaaluma akitoa elimu kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Kurugenzi yake na faida ya CPA na kuwa mwanachama wa Bodi.
Magreth Kageya, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa NBAA akitoa mada kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na NBAA "NBAA Overview" kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Baobab waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
CPA George Lazaro, Mkaguzi wa ndani wa NBAA akitoa elimu kuhusu Ukaguzi na majukumu mbalimbali ya Mkaguzi kwa wanafunzi wa Kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Baobab Stephen Mahundi akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) walipotembelea ofisi za Bodi ya NBAA.
Baadhi ya wafanyakazi wa NBAA na wanafunzi wa Kidato cha Tano wanaosoma masomo ya Biashara katika Shule ya Sekondari ya Baobab wakifuatilia mada kwa wataalam kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) walipotembelea ofisi za Bodi hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi (waliokaa, katikati) kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wafanyakazi wa Bodi hiyo, walimu na wanafunzi wa Kidato cha Tano wanaosoma masomo ya Biashara kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab walipotembelea ofisi za NBAA kwa ajili ya kupata elimu.

No comments