Header Ads

test

SERIKALI KUONGEZA KASI YA UANDAAJI MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI VIJIJINI

Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi nchini, Serikali imelenga kutekeleza mikakati ya kuongeza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi vijijini pamoja na kutumia mbinu jumuishi na shirikishi zinazowahusisha wananchi na wadau katika hatua za upangaji wa ardhi.

Mikakati hiyo inalenga kutekelezwa kwa kupanua programu za kitaifa za upangaji ardhi vijijini kwa kushirikiana na wadau wa maeneo husika, kutumia teknolojia za kisasa na ramani za kidigitali ili kuongeza ufanisi, pamoja na kuharakisha upimaji na utoaji wa hati za kimila, kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi.

Akizungumza wakati wa kuzindua jukwaa la siku tatu la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi mkoani Morogoro tarehe 12 Mei 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, alisema mikakati hiyo pia inahusisha kuimarisha ushirikiano kati ya wizara, halmashauri, wadau na jamii kwa ujumla katika utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo.

Amesema serikali inahamasisha matumizi endelevu ya ardhi, ikiwemo kilimo hifadhi na ufugaji unaozingatia uwezo wa ardhi, ili kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa tija na kwa njia inayopunguza migogoro.

Kwa ujumla, Mhe. Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa mikakati hiyo inalenga kuleta mabadiliko kutoka katika hatua ya kupanga mipango kwenda katika utekelezaji wake kwa vitendo, ili kuhakikisha ardhi inatumika kwa njia jumuishi inayozingatia maendeleo endelevu.

Ametoa rai kwa jamii kushiriki kuchangia gharama za uandaaji wa hati za hatimilki za kimila, kama ambavyo tayari imeanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo na kusisitiza kuwa, utaratibu huo utasaidia kuongeza kasi ya umilikishaji wa ardhi na kuwafanya wananchi kuwa na milki salama.

“Bila shaka, uchangiaji huu wa gharama utaongeza kasi ya umilikishwaji na hivyo kuwafanya wananchi kuwa na milki salama,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, alisema mkoa wake umechukua hatua madhubuti katika kukabiliana na migogoro ya ardhi, hususan kati ya wakulima na wafugaji, kwa kufanya tathmini na utafiti wa kina kubaini chanzo cha changamoto hizo.

Amesema mkoa wa Morogoro umeweka utaratibu wa kujadili migogoro ya wakulima na wafugaji kama ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa vinavyofanyika kila mwezi.

“Tumefanya maamuzi ya makusudi ya kuhakikisha tunabaini tumetokea wapi. Katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, kila mwezi tumeweka ajenda ya migogoro ya wakulima na wafugaji,” alisema Mhe. Malima.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Joseph Mafuru, alisema takwimu zinaonesha kuwa kati ya vijiji 12,333 nchini, ni vijiji 4,925 pekee, sawa na asilimia 39.9, ndivyo vilivyo na mipango ya matumizi ya ardhi, huku vijiji 7,408 bado havijapata mipango hiyo.

Bw. Mafuru alisema changamoto kuu zinazosababisha kasi ndogo ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni ufinyu wa rasilimali fedha na matumizi hafifu ya teknolojia stahiki.

Ameeleza kuwa, licha ya kuongezewa bajeti kila mwaka, bado kuna haja ya wadau mbalimbali kukutana na kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha kukamilisha hatua zote za upangaji wa matumizi ya ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kuzindua jukwaa la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi lililofanyika mkoani Morogoro tarehe 12 Mei 2026.

Sehemu ya washiriki wa jukwaa la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Wa pili kushoto) na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (kushoto) wakipata maelezo ya vitabu vinavyoelezea mipango ya matumizi ya ardhi kutoka kwa Afisa Mipango Miji Mkuu wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bw, John Chua wakati wa Jukwaa la wadau lililofanyika mkoani Morogoro tarehe 12 Mei 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima akizungumza katika Jukwaa la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi linaloendelea mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Tume ya Matumizi bora ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi lililofanyika mkoani Morogoro.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Wa pili kulia), Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (kulia) na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru (kulia) wakifuatilia michango ya wadau wakati wa uzinduzi wa jukwaa la wadau wanaohusika na uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi uliofanyika mkoani Morogoro ( PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments