TANZANIA NA KENYA KUONDOA VIKWAZO VISIVYO VYA KODI
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kikodi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ili kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 04, 2026 mara baada ya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, aliyewasili nchini kwa ziara ya kitaifa, Rais Samia amesema mazungumzo yao yamelenga zaidi masuala ya kiuchumi yanayogusa ustawi wa mataifa hayo.
Amesema Kamati za Pamoja za Biashara kati ya Tanzania na Kenya zitaendelea kukutana mara kwa mara kujadili changamoto za kibiashara na kuhakikisha hakuna vikwazo vipya vinavyojitokeza, hatua inayotarajiwa kurahisisha biashara ya mipakani.
Katika ziara hiyo, mikataba nane imesainiwa ikihusisha sekta za nishati, miundombinu na uchukuzi, ulinzi, TEHAMA ambapo Rais Samia ameeleza kuwa katika sekta ya nishati, nchi hizo zimekubaliana kuendelea na miradi ya kuunganisha umeme, ambapo njia moja tayari imekamilika huku maandalizi ya ujenzi wa njia ya pili yakiendelea.
Kwa upande wa miundombinu, amebainisha kuwa makubaliano yamefikiwa ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, pamoja na kuunganisha reli kutoka Bandari ya Tanga kupitia Kilimanjaro hadi Kenya. Pia, Kenya itaunganisha reli yake na kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) cha Tanzania kutoka Singida.
Aidha, nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria ili kurahisisha biashara inayohusisha Tanzania, Kenya na Uganda.




Post a Comment