Header Ads

test

UJIO KOCHA BEN LEE WAIPA TANZANIA FURSA KUINUA MCHEZO WA UOGELEAJI

Na Mwandishi Wetu, 

TANZANIA  imepiga hatua nyingine katika juhudi za kuendeleza mchezo wa uogeleaji kufuatia kuwasili kwa kocha wa kimataifa, Ben Lee, ambaye atatoa mafunzo ya kiwango cha kimataifa kwa waogeleaji, makocha na wazazi kupitia programu maalumu iliyoandaliwa na Monti International School.

Ujio wa Ben Lee unaelezwa kuwa ni hatua muhimu katika safari ya kuinua viwango vya uogeleaji nchini kwa kuwaletea Watanzania utaalamu wa kimataifa bila kulazimika kusafiri nje ya nchi. Kocha huyo ana uzoefu mkubwa wa kuwafundisha waogeleaji walioshiriki mashindano ya NCAA na Olimpiki.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mapokezi ya kocha huyo jana jijini Dar es Salaam, Afisa Michezo wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Petro Gallos mbali na kupongeza ujio wake, amesema wakufunzi wa ndani wa mchezo huo wanapaswa kutumia mwanya huo adhimu kwa kuchota ujuzi wenye manufaa.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), Amina Mfaume alisema; “mafunzo yatakayotolewa na kocha huyo yataongeza ufanisi wa makocha wetu na kutusaidia kuangalia maendeleo ya waogeleaji kwani wale watakaowashiriki wataona jinsi gani makocha wa kimataifa wanavyofanya mafunzo yao.”

Awali Mkurugenzi wa Monti International School, Fatma Fernandes, alisema ushirikiano kati ya RaceBetter na Monti si wa tukio la muda mfupi, bali ni mwanzo wa mpango wa muda mrefu unaolenga kuendeleza vipaji vya waogeleaji wa Tanzania na kuwajengea uwezo makocha wa ndani.

"Ujio wa Ben Lee nchini Tanzania ni hatua muhimu katika safari yetu ya kuijenga Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya uogeleaji Afrika Mashariki. Kupitia ushirikiano huu, tunataka kuwajengea uwezo waogeleaji, makocha na wazazi, na kuweka msingi imara wa mafanikio ya muda mrefu katika mchezo wa uogeleaji," alisema Fatma Fernandes.

Kwa mujibu wa ratiba ya programu hiyo, mafunzo kwa makocha yatafanyika kuanzia Julai 28 hadi 30, yakifuatiwa na kambi za mafunzo kwa waogeleaji wa makundi mbalimbali ya umri, huku mafunzo ya juu yakihitimishwa Agosti 14.

Fernandez alisema mafunzo kwa makocha yatatolewa bure kwa makocha wote waliosajiliwa na Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), licha ya gharama za kumleta kocha huyo wa kimataifa kugharamiwa kikamilifu na Shule ya Kimataifa ya Monti.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatafanyika katika bwawa la kisasa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Monti, Mikocheni, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi kila siku.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili nchini Tanzania, Ben Lee mbali nakushukuru kwa mapokezi makubwa, alisema ujio wake unalenga kusaidia kuendeleza vipaji vya wazawa kuanzia ngazi za chini na kuweka misingi kwa makocha na waogeleaji kupata mafanikio ya muda mrefu.



 

No comments