TASAF YATAKIWA KUJENGA UWEZO WA WANANCHI KUJITEGEMEA
Serikali imeutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha programu zinazowawezesha wananchi kujitegemea badala ya kujikita katika utoaji wa misaada ya kijamii.
Akizungumza leo Agosti 6, 2026 Jijini Dar es salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray, amesema Dira 2050 inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaoinua maisha ya kila mwananchi, hivyo TASAF inapaswa kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.
“TASAF iondokane na dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba jukumu lake ni kutoa misaada ya kijamii pekee, na badala yake ijikite katika kuwawezesha wananchi kujenga uwezo wa kujitegemea kupitia shughuli zenye tija zinazoongeza kipato cha kaya”. amesema.
Aidha, amesema TASAF inasimamia rasilimali kubwa za umma zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa fedha za umma ili kuzuia ubadhirifu, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa programu na kuhakikisha uwajibikaji katika ngazi zote.
Sambamba na hayo, ametoa wito kwa TASAF kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijiti inayowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu na matokeo yake kwa wakati halisi, hatua itakayorahisisha kufanya maamuzi kwa kuzingatia takwimu sahihi na kuongeza uwajibikaji.
Vilevile, amesema ni muhimu kuendelea kuimarisha usalama wa taarifa za walengwa kwa kuzingatia viwango vya usalama wa mifumo ya TEHAMA na ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo kujenga imani ya wananchi, kulinda faragha zao na kuhakikisha mifumo ya TASAF inabaki kuwa salama, ya kuaminika na endelevu.


.jpeg)



Post a Comment