Header Ads

test

WAZIRI WA ARDHI DKT AKWILAPO AINGIA ‘SITE’ KUTAFUTA SULUHU YA MIGOGORO YA ARDHI MKOANI TANGA


Na Munir Shemweta,Tanga

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amefanya ziara katika maeneo yenye migogoro ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga, kwa lengo la kupata undani wa migogoro hiyo baada ya kupokea malalamiko.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro ya ardhi nchini.

Akiwa jijini Tanga tarehe 19 Agosti 2026, Dkt. Akwilapo alianza ziara yake katika eneo la Raskazone ambako alikagua mgogoro unaohusisha Kiwanja Na. 163, Kitalu KB XVI, ambapo mmiliki wake anadai kuwa sehemu ya barabara inayoelekea kwenye ofisi za kampuni ya GBP, imejengwa katika eneo la kiwanja chake. Waziri huyo pia alitembelea eneo la Chumvini, Kata ya Chumbageni, ambako baadhi ya wananchi wanadaiwa kufanya maendelezo ndani ya eneo la hifadhi ya mikoko.

Baadaye, Dkt. Akwilapo alielekea wilayani Handeni na kutembelea maeneo mbalimbali yenye malalamiko ya ardhi katika kata za Kwenjugo, Chanika na Mdoe. Akiwa katika maeneo hayo, alipokea maelezo kutoka kwa madiwani na viongozi wa maeneo husika kuhusu migogoro iliyodumu kwa muda na kusababisha sintofahamu miongoni mwa wananchi, huku akijionea hali halisi ya maeneo yanayolalamikiwa.

Miongoni mwa migogoro aliyoikagua ni ule kati ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) cha Handeni na kampuni ya Lyakundi Investment, ambapo kampuni hiyo inadaiwa kumilikishwa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 21,937 badala ya mita za mraba 5,625, hali inayodaiwa kuingia katika eneo linalomilikiwa na chuo hicho.

Dkt. Akwilapo pia alitembelea eneo jirani na Shule ya Msingi Mshikamano, ambako kampuni hiyo ya Lyakundi Investment imezuiwa na Halmashauri ya Mji Handeni kuendeleza kiwanja kufuatia malalamiko ya wananchi na viongozi wao kwamba taratibu za umilikishaji wa eneo hilo hazikuzingatia kanuni.

Katika mwendelezo wa ziara hiyo, Waziri Akwilapo alikagua eneo la Milupi lenye mgogoro kati ya familia ya marehemu Yusuf Ulenge na uongozi wa Mtaa wa Ngugwini kuhusu umiliki wa eneo la ekari 15. Pia alitembelea eneo la Seuta, ambako Diwani wa Kata ya Kwenjugo, Bw. Twaha Mgaya, alieleza kuwa baadhi ya viwanja vimemilikishwa kwa watu bila kufuata taratibu , Waziri pia alitembelea eneo la Kwedisewa.

Eneo jingine alilokagua Dkt. Akwilapo ni lenye mgogoro kati ya Halmashauri ya Mji Handeni na familia ya Hassan Msindo, ambayo inadaiwa kuwa eneo lao la ekari 30 lilipimwa na kugawanywa kuwa viwanja, lakini badala ya familia hiyo kupatiwa asilimia 60 ya eneo inalodai kumiliki, ilipatiwa viwanja vitatu pekee. Familia hiyo imeeleza kutoridhishwa na hatua hiyo na kuiomba Serikali kuingilia kati ili kupatikana suluhu ya haki.

Wakati wa kuhitimisha ziara hiyo Mhe, Dkt Leonard Akwilapo alisistiza umuhimu wa taasisi, viongozi na wananchi kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za usimamizi na umiliki wa ardhi ili kuzuia migogoro. Hatua hiyo inaendana na moja ya vipaumbele sita vya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi vilivyoainishwa na Waziri huyo wakati wa Bunge la Bajeti 2026/2027, ambacho ni uimarishaji wa mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi. 

Aidha aliwapongeza viongozi wa mikoa na wilaya kwa nchi nzima kwa kuisaida wizara katika kushugulikia migogoro ya ardhi katika maeneo yao ya utawala. Waziri alihitimisha kwa kuahidi kutoa maelekezo ya utatuzi wa migogoro aliyiotembelea katika muda mfupi ujao ili wenye haki waendelee na uendelezaji wa maeneo yao.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (wa pili kushoto), Mkuu wa wilaya ya Handeni Salum Nyamwese (kushoto) wakioneshwa moja ya eneo lenye mgogoro wa ardhi katika kata ya Chanika kupitia ‘laptop’ na Afisa Ardhi Mwandimizi wa Wizara ya Ardhi Bw. James Balele wakati wa ziara yake wilayani Handeni. Kushoto ni Diwani wa kata ya Chanika Halmashauri ya Mji Handeni Habib Mbota.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (wa tatu kushoto) akioneshwa eneo la mgogoro katika kata ya Chanika na Afisa Ardhi Mwandimizi wa wizara ya Ardhi Bw. James Balele wakati wa ziara yake wilayani Handeni. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Handeni Salum Nyamwese.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Katikati), Mkuu wa wilaya ya HandeniSalum Nyamwese (kushoto) na Diwani wa kata ya Chanika Halamshauri ya Mji Handeni Habib Mbota wakielekea katika moja ya eneo lenye mgogoro wa ardhi wakati wa ziara ya Waziri wilayani handeni jana.Diwani wa Kata ya Kwenjugo Bw, Twaha Mgaya akisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Ardh,i Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo alipofanya ziara wilayani Handeni kushughulikia changamoto za migogoro ya ardhi jana.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (wa pili kushoto) akioongozwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tanga Jabir Singano alipotembelea eneo lenye mgogoro wa ardhi eneo la Raskazone Tanga wakati wa ziara yake mkoani humo jana.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akioneshwa eneo la Chumvini, Kata ya Chumbageni na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tanga Jabir Singano ambako baadhi ya wananchi wanadaiwa kufanya maendelezo ndani ya eneo la hifadhi ya mikoko (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

No comments