Header Ads

test

DAWA ZA MILIONI 360 ZANASWA JNIA, WATU 5 WAKAMATWA

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba nchini TMDA imefanikiwa kunasa shehena mbili kubwa za dawa na vifaa tiba zisizo sajiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere JNIA Terminal 3. Thamani ya jumla ya mizigo hiyo inakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 360.Akizungumza na vyombo vya habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo amesema shehena ya kwanza ilikamatwa tarehe 7 Septemba 2026 wakati wakaguzi wao wakifanya ukaguzi wa kawaida kupitia mfumo wao wa udhibiti.


"Wakaguzi wetu wamefanikiwa kukamata mabegi 20 yaliyokuja kutoka India. Yalikuwa na dawa nyingi sana zenye thamani ya shilingi milioni 310. Hapakuwa na nguo wala vyakula. Tatizo kubwa ni kwamba dawa hizo zote hazikuwa na usajili wala vibali vyovyote vya TMDA," amesema Dkt. Fimbo.
Dkt. Fimbo ameongeza kuwa tarehe 9 Septemba 2026, wamefanikiwa tena kunasa shehena nyingine yenye thamani ya shilingi milioni 50. Ndani ya shehena hiyo kulikuwa na sindano za lignocaine, bupivacaine, adrenaline na vitamini.

Pia kulikuwa na dawa za kutibu magonjwa ya saratani, kifafa, shinikizo la damu na kisukari. Miongoni mwa dawa hizo ni OZEMPIC na GLP-1 ambazo ni sindano maarufu sasa hivi mitandaoni zinazotumika kupunguza unene. Shehena hiyo pia ilikuwa na vifaa tiba vya meno bandia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, dawa zisizosajiliwa ni hatari kubwa kwa afya ya wananchi kwani ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa na TMDA. Matumizi yake yanaweza kusababisha madhara kama kuchelewa kupona, usugu wa dawa, ulemavu na hata vifo.

Dkt. Fimbo amebainisha kuwa mpaka sasa watu watano wameshakamatwa na vyombo vya usalama na bado wanaendelea na uchunguzi zaidi. Amesisitiza kuwa dawa zote zilizokamatwa zitaenda kuteketezwa mara tu uchunguzi utakapokamilika.

TMDA imetoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuzingatia sheria na taratibu za uingizaji na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Amesema ni marufuku kuingiza bidhaa za tiba bila kupata kibali cha TMDA na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote.




 

No comments