Header Ads

test

SERIKALI YAAGIZA UKAGUZI MAENEO YA UWEKEZAJI NCHINI

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewaagiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi katika mikoa yote nchini kufanya ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo yasiyoendelezwa na kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe

Dkt. Akwilapo ametoa agizo hilo Septemba 18, 2026, mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika maeneo ya uwekezaji ya Kongani ya Viwanda ya KAMAKA pamoja na kiwanda cha Nondo cha Gain Company Limited kilichopo Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Amesema Wizara ya Ardhi, imebaini kuwepo kwa maeneo ambayo yalipewa wawekezaji kwa ahadi ya kuanzisha viwanda au shughuli nyingine za uzalishaji, lakini hayajaendelezwa kwa muda uliokubaliwa.

“Tuna taarifa kuna waliochukua maeneo wakasema watatengeneza viwanda lakini bado hawajafanya hivyo. Natoa maelekezo makamishna kufanya ukaguzi na kuwasilisha taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa maeneo yasiyoendelezwa kadri ya mikataba waliyoingia,” amesema Dkt. Akwilapo.

Aidha, Waziri huyo amewataka wamiliki wote wa ardhi ambao hawazingatii masharti ya uendelezaji maeneo waliyopewa kuhakikisha wanayaendeleza kwa wakati, vinginevyo wizara itachukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Amesisitiza kuwa, hatua hizo zitawahusu wawekezaji wazawa na wa kigeni, akieleza kuwa kwa wawekezaji wazawa hatua inaweza kujumuisha kubadilisha milki za ardhi walizopewa, huku kwa wawekezaji wa kigeni wizara ikishirikiana na taasisi husika, ikiwemo TISEZA, katika kushughulikia masuala ya umiliki na uwekezaji.

Dkt. Akwilapo amesema, hatua hiyo inalenga pia kujibu malalamiko kutoka kwa wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya uwekezaji, lakini baadaye hayakuendelezwa.

Ameeleza kuwa, hali hiyo imekuwa ikisababisha wananchi kuhoji sababu za maeneo kutolewa kwa wawekezaji ambao hawajaanza shughuli za maendeleo kwa muda mrefu.

Awali Mhe Dkt Akwilapo alielezwa kuwa eneo la Kongani ya Viwanda Mlandizi wilayani Kibaha mkoa wa Pwani linakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile upatikanaji wa maji na ubovu wa barabara hali waliyoieleza kuwa inayosababisha kero katika usafirishaji bidhaa na malighafi.

Hata hivyo, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wameeleza kuanza  kuchukua hatua za dharura kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu

Ziara ya Dkt. Akwilapo katika Mkoa wa Pwani imelenga kujionea kwa karibu shughuli za uwekezaji na matumizi ya ardhi katika maeneo hayo, pamoja na kutathmini namna bora ya kuendeleza maeneo ya uwekezaji kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na maendeleo endelevu.

Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za kutambua fursa na changamoto zinazohusiana na ardhi na uwekezaji, kwa lengo la kuimarisha matumizi bora ya ardhi, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ziara yake kutembelea Kongani ya Viwanda ya KAMAKA pamoja na kiwanda cha Nondo cha Gain Company Limited Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani Sept 18, 2026. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bw. Nickson Simon na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa KAMAKA Bw, Yusuf ManziMkuu wa mkoa wa Pwani Mhe, Stanslaus Nyongo akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo kutembelea Kongani ya Viwanda ya KAMAKA pamoja na kiwanda cha Nondo cha Gain Company Limited Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani Sept 18, 2026.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akipata maelezo kuhusiana na kituo kidogo cha kudhibiti umeme kilichopo eneo la Kongani ya viwanda Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani kutoka kwa Meneja wa Mradi Bw. Leonard Paul Sept 18, 2026.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiwa katika kiwanda cha Nondo cha Gain Company Limited wakati wa ziara yake ya kutembelea eneo la Kongani ya viwanda Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani Sept 18, 2026.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Katikati) akiwa katika picha ya Pamoja na viongozi mbalimbali mkoani Pwani alipotembelea Kongani ya Viwanda ya KAMAKA Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani Sept 18, 2026. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Bw. Nickson Simon (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI) 

No comments