WANAFUNZIA 5,924,803 WAFIKIWA NA MRADI WA USOMAJI NA MAKTABA
Na Mwandishi Wetu, Dar
SHIRIKA la Room to Read Tanzania limesema takribani Wanafunzia 5,924,803 wamefikiwa na Mradi wa Usomaji na Maktaba huku wengine 26,437 wakinufaika na Mradi wa Usawa wa Kijinsia katika shule mbalimbali nchini zinazotekeleza miradi hiyo.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Afisa Mwandamizi Mradi wa Usomaji na Maktaba kutoka Shirika la Room to Read Tanzania, Mwalimu Veronica Mahenge kwenye Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA) lililofanyika kwa suku nne mfululizo, alisema lengo ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi ili kuhakikisha wanapomaliza elimu ya Sekondari wanakuwa na stadi za msingi za maisha zitakazomsaidia mwanafunzi kupambana na changamoto anuai kabla ya kufikia malengo yake.
Akifafanua zaidi, Mwl. Mahenge alisema kutekeleza mradi wa Usomaji na Maktaba Shirika la Room to Read linashirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba watoto wanajenga stadi za kusoma na kuandika kwa wakati kwa kutoa mafunzo kwa walimu na kutoa usaidizi wa kitalam shuleni, pia kuwashirikisha wana jamii kwa karibu zaidi.
"..Katika kutekeleza mradi huu tuna kipengele maalum kinaitwa ushirikishwaji wa familia na jamii, ambapo tunafanya kazi kwa karibu na jamii...Yote haya ni kuhakikisha watoto kupitia usaidizi wa walimu pamoja na mzazi wanaweza kufikia malengo, ambayo ni kusoma na kuandika kwa wakati. Pia katika mradi huu tunaboresha na kuhimarisha stadi za usomaji na kuandika kupitia maktaba za shule," alieleza Mwl. Mahenge.
Aidha aliongeza kuwa mradi wa usomaji na maktaba unahimiza ushirikishwaji wa familia na jamii kwenye eneo la maktaba, huku ukiitaka jamii kutambua kuwa maktaba si kwa ajili ya watoto tu, bali hata wazazi wanaweza kuzitumia ili kuweza kuwasaidia watoto kuzifikia fursa za kupata vitabu na kwenda kujisomea wawapo nyumbani, kwani lengo ni kuwasaidia watoto kujenga tabia za usomaji, hasa kupitia mfumo wa maktaba mtandao (Online Library).
Naye Afisa Ufundi wa Room to Read, Bi. Tafatia Malogo akizungumzia mradi wa Usawa wa Kijinsia alisema ulianza kutekelezwa Mvomero katika Shule za Sekondari na baadaye kwenda Wilaya ya Bagamoyo katika Kata za Zinga, Kiromo, Chalinze, Kingani na Lugoba; kabla ya kuendelea Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.
![]() |
| Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA) lililofanyika jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye mkutano wa kongamano hilo. |
Aidha alisema kwa sasa mradi huo unatekelezwa Mkoani Tanga katika Wilaya za Handeni, Muheza na Tanga Jiji, pamoja na baadhi ya Shule za Mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar huku ukiwajumuisha pia wanafunzi wa kiume tofauti na awali ulipokuwa umewalenga zaidi wasichana pekee, katika shule za sekondari.
Alibainisha kuwa, Mradi wa kijinsia umejikita kuhakikisha kwamba wanafunzi wanamaliza elimu ya sekondari huku wakiwa na stadi tano za maisha zikiwemo, ushirikiano, kufanya uamuzi, ustahimilivu, uongozi pamoja na fikra tunduizi. aliongeza kuwa lengo katika mradi huu ni kuona nchi inakuwa kizazi cha vijana walioelimika, yaani kujua kusoma na kuandika, chenye kujali usawa wa kijinsia na uwezo wa kufanya maamuzi ya msingi katika maisha yao.




Post a Comment