SERIKALI YATENGA BILIONI 9.4 KUKABILIANA NA ONGEZEKO LA MAHITAJI YA MAJI JIJINI DODOMA
Na Janeth Raphael.
Katika kukabiliana na ongezeko kubwa la mahitaji ya maji katika jijini la Dodoma Serikali kupitia Wizara ya maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) imewekeza kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 9.14 kwa hatua za muda mfupi za kukabiliana na uhaba wa maji jijini humo.
Mkurugenzi Mtendaji DUWASA Mhandisi Aron Joseph ameyaeleza hayo leo katika mkutano na wanahabari wakati akitoa taarifa yake ya mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika kupindi cha miaka miwili kwenye Sekta ya maji jijini Dodoma.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) imefikia mafanikio mbalimbali katika kupindi cha miaka miwili ya Rais Dkt Samia Suluhu hassan ambapo ongezeko la uzalishaji maji kutoka wastani wa lita milioni 61.5 na kufikia lita milioni 67.1 Kwa siku.
"Jukumu la msingi la Duwasa ni kutoa huduma ya majisafi na uondoaji majitaka kwa wakazi wa miji ya chamwino, Kongwa na Bahi, takribani asilimia 91 ya wananchi wanapata huduma ya Majisafi na salama ( kwa mgao) na asilimia 20 wanapata huduma ya uondoshaji wa majitaka. " - amesema Mhandis Aron
Kwa upande wa majitaka Mhandisi Aron amesema Serikali imetenga kiasi cha Bilioni 4.9 kwa ajili ya kukarabati mtambo wa maji taka eneo la Area D na C, kukarabati kilometa 19 za mtambo chakavu , ujenzi wa chemba 1,005 kuhamisha wateja kwenye mtandao mpya na hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 86 ya utekelezaji.
Mhandisi Aron amesema tayari uchimbaji wa visima 32 kutoka sehemu mbalimbali za huduma, ufungaji wa pampu, ulazaji wa kilometa 208.86 za mtandao wa kusafirisha na kusambazia maji, pamoja na ujenzi wa matenki yenye ujazo wa lita 3,035,000 hayo yameshafanyika.
Aidha katika mradi wa dharura Mhandisi Aron amesema Mpango wa dharura uliyopo kwa sasa ni mradi wa maji kutoka bwawa la Mtera ambapo unatarajiwa kuleta lita za maji milioni 130 kwa siku na jumla ya fedha za Kitanzania bilioni 326 zitatumika na benki ya Dunia imeinyesha nia ya kufadhili mradi huo.
"Katika mradi huu Mhandisi mshauri atawasilisha taarifa yake ya mwisho ifikapo mwezi machi mwaka huu 2023 na mradi huu unaweza kujegwa ndani ya kipindi cha miaka miwili" - amesema Mhandisi Aron
Hata hiyo Mhandisi Aron amesema katika mafanikio hapakosekani changamoto
zipo nyingi sana hasa kwenye upande wa matumizi sahihi ya maji taka mitaro mingi mafudi wanapoenda kuzibua wanakutana na vitaulo (pedi za matumizi ya wanawake), sox, mipira ya wanaume ( condom)
"Kwa kweli tunajiuliza hii ni sehemu sahihi ya kutupa vitu hiyo? mtandao wa maji taka ni kwa ajili ya maji taka pekee na ili iweze kwenda sawa ndiyo maana zilitengenezwa karatasi laini (tissue) ambayo inayeyuka sasa mtu anachukua gunzi la mahindi anatumbukiza katika shimo la choo litayeyukaje? na likifika mbele likagota huyo huyo ndiye wa kwanza kulalamika sio sawa hiyo kwetu ni changamoto kubwa inayotukabili." amesema Mhandisi Aron.
Mhandisi Aron ametoa wito kwa wananchi kuwa na matumizi sahihi ya maji ili kupunguza kupata malalamiko ya kupata bili kubwa wakati wa kufanya malipo kila mwezi.
Post a Comment