Header Ads

test

MAKALA KILIMO CHA BUSTANI

 

Na Mwandishi Wetu

Matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 nchini Tanzania
yalibainisha kuwa, asilimia 34.5 ya watanzania wote ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa. Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha vijana
wanahusishwa kikamilifu katika miradi na programu za maendeleo kupitia mafunzo
ya ujuzi na Ufundi stadi ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana katika ngazi zote.


Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuunga mkono jitihada hizo za Serikali,
ilitoa ruzuku kwa ajili ya Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi katika sekta ya Kilimo kupitia
Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), kwa Taasisi inayojihusisha na Kilimo-Biashara
cha Bustani na Mbogamboga (TAHA) mwaka 2021 kwa lengo la kunufaisha vijana
400 kwa kuwajengea uwezo kuhusu kilimo cha bustani (horticulture).

Kupitia ruzuku hiyo ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), jumla ya vijana 437
wamenufaika na mafunzo hayo ambayo yalifanyika katika maeneo mbalimbali ya
Jijini Arusha yakitolewa na Taasisi ya TAHA na hadi sasa asilimia 90 ya vijana hao
ni wakulima wakubwa wa mbogamboga na matunda wanaofurahia soko la ndani na
nje ya Tanzania.

Gilliad Daniel Kiongozi wa Uzalishaji (Production Lead) kutoka TAHA anasema, ruzuku waliyopewa kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) imeleta mabadiliko
chanya ndani ya Taasisi yao kupitia programu ya kuendesha mafunzo ya kuwajengea vijana uwezo katika Kilimo cha Bustani baada ya muitikio kuwa mkubwa tofauti na walivyotarajia.

‘‘Makubaliano ya mradi yalikuwa ni kuwafikia vijana 400 hadi unakamilika kwa
maana ya kutoa mafunzo ila tulishangaa vijana walivyochangamkia fursa hiyo,
mwisho tukafundisha 37 zaidi na hivyo kuwa na idadi ya wanufaika 437, alisema
Gilliad’’

Aidha, TEA ilitoa ruzuku kwa Taasisi ya TAHA kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi
(SDF) kwa lengo la kufadhili mafunzo ya ujuzi kwa vijana katika Sekta ya Kilimo
kama moja ya sekta za kipaombele ikizingatia kuwa, sekta hii ina mchango mkubwa
katika uchumi wa Tanzania. Takwimu na machapisho mbalimbali yamekuwa
yakionyesha kuwa asilimia 90 ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo
na sekta ya kilimo inatoa ajira kwa asilimia 65.5 na inachangia asilimia 29.1 ya pato
la Taifa, asilimia 30 ya soko la nje na asilimia 65 ya malighafi za viwandani
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati
Geuzye alifanya ziara ya kikazi Jijini Arusha mwanzoni mwa wiki kwa lengo la
kukutana na uongozi wa TAHA lakini pia kuwatembelea baadhi ya wanufaika wa
mafunzo hayo ya ujuzi kuona maendeleo yao baada ya kujengewa uwezo kupitia
ruzuku ya Mfuko wa SDF

Katika ziara hiyo, Geuzye alifurahia kuona wanufaika wanaendeleza kilimo kwa
kutumia utaalam walioupata chini ya TAHA lakini pia alifarijika kusikia kwamba kwao
soko siyo changamoto tena maana mafunzo waliyopatiwa yanawasaidia kuzalisha
bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji ya soko.

‘‘Nafarijika sana kuona hamkurudi nyuma baada ya mafunzo maana vijana wengi
hawapendi kazi za kilimo kutokana na changamoto mbalimbali. Ni wakati muafaka
sasa vijana wengine wajifunze kuthubutu na kutokukata tamaa kupitia kwenu
mliofanikiwa katika sekta hii, alisema Geuzye’’
Geuzye aliongeza kwamba, Serikali inatambua mchango wa vijana katika kukuza
uchumi wa nchi lakini pia mchango wa sekta ya kilimo katika kukuza pato la Taifa.


Ndiyo maana vijana wanahamasishwa kuwekeza kwenye sekta hii, kupitia fursa
mbalimbali zinazotolewa na Serikali, wadau na Sekta binafsi kwani kilimo ni muhimili wa maendeleo kwa nchi yetu.

Lugano Ipyana mmoja wa wanufaika alithibitisha hayo kwanza kwa kuishukuru
Serikali kwa kuwathamini vijana kisha akasema, yeye alisoma hadi ngazi ya
stashahada na kufanikiwa kufanya kazi na makampuni mbalimbali ya watu binafsi ila hakuridhika na kipato alichokuwa akipata kazini kwake hivyo aliamua kutafuta kitu kingine cha ziada cha kumuongezea kipato.

Ipyana anafafanua kwamba, mwaka 2021 alisikia tangazo la kuwezesha vijana
kuwajengea uwezo kufanya kilimo cha bustani lililotolewa na TAHA na bila kusita
alituma maombi akafanikiwa kuchaguliwa. Mafunzo yalikuwa ya muda mfupi na
walijikita zaidi kwenye mafunzo kwa vitendo kitu ambacho kilimjengea uwezo wa
kujiamini katika kile alichokuwa anakifanya.

Anafafanua kwamba, wakati wa mafunzo alikuwa na shamba lenye ukubwa wa ekari
moja na ndilo alilolitumia kama shamba la majaribio kwa kulima nyanya na pilipili
hoho. Wataalam wa kilimo cha bustani kutoka TAHA walimfungia miundombinu ya
umwagiliaji na wakamuwezesha pembejeo zikiwemo mbegu na madawa na baadae
wakamuunganisha na masoko kwa ajili ya kuuza mazao yake.

‘‘Kwa sasa nina zaidi ya ekari 5 ambazo ninaweza kulima aina 5 za mazao kwa
wakati mmoja. Pia nashukuru nilikuwa natamani sana kuzalisha bidhaa kwa ajili ya
soko la nje na nimefanikiwa, mara ya kwanza nililima maharage (French Beans)
nikapata tani 2 ambazo niliuza takribani milioni 16, alisema Ipyana’’.

Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na TEA umeleta mabadiliko chanya
kwa vijana kupitia mafunzo ya elimu ya ufundi na stadi za kazi. Takribani vijana
35,000,000 wamenufaika na mafunzo hayo katika sekta sita za kipaombele. Sekta
hizo ni utalii na huduma za ukarimu, nishati, kilimo biashara, ujenzi, uchukukuzi na TEHAMA.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye (wa tatu kulia)
pamoja na wataalam wa kilimo kutoka TAHA wakikagua mmea wa nyanya kwenye
shamba la mnufaika wa Mafunzo ya Ujuzi Jijini Arusha.


No comments