Header Ads

test

MRADI WA BOOST WAIWEZESHA TSC KUANZA KUPITIA SHERIA ZOTE ZINAZOMGUSA MWALIMU

 

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeanza mchakato wa kupitia sheria na kanuni zote zinazomsimamia mwalimu ili kufanya maboresho katika kumhudumia mwalimu kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia rasimu ya mapendekezo yaliyoandaliwa na timu ya wataalamu wa sheria, elimu na usimamizi wa rasilimali watu baada ya kupitia sheria hizo, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amesema kazi hiyo inafanyika kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa BOOST ambao unafadhili shughuli mbalimbali za elimu nchini.

Kikao kazi hicho kinaikutanisha Menejimeti ya TSC na timu ya wataalamu hao na kinafanyia kwa siku tatu kuanzia Machi 1 hadi 3, 2023 katika ukumbi wa Mahakama mjini Morogoro.

Mwl. Nkwama amefafanua kuwa mradi wa BOOST una afua nane (8) na moja ya afua hizo ni Shule Salama ambapo TSC ni miongoni mwa wanufaika kwa kuwezeshwa kuandaa miongozo na nyaraka mbalimbali za kusimamia utumishi wa walimu, kutoa mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya walimu, kununua vitendea kazi ikiwemo magari na kompyuta.

Ameongeza kuwa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ufadhili wa mradi huo ni matokeo ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutafuta wadau wa maendeleo kwa ajili ya kuleta mageuzi katika sekta ya elimu kwa lengo la kumfanya mwalimu aweze kutoa huduma bora ya kuwalea wanafunzi katika nyanja zote kama ilivyokusudiwa.

“Tupo hapa kwa ajili ya kufanya mapitio ya mapendekezo yanayotokana na kazi inayoendelea kufanyika ya kupitia sheria mbalimbali zinazomgusa mwalimu na utumishi wake kwa ujumla. Haya yote tunayafanya kwa lengo la kutafuta njia nzuri itakayomfanya mwalimu aifurahie kazi yake na atekeleze majukumu yake kwa amani, utulivu na ufanisi zaidi,” amesema.

Katibu huyo ameweka wazi kuwa maboresho mbalimbali yanayofanyika kwenye sekta ya elimu yanalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi inayotoa elimu bora kitaifa na kimataifa, na mtoto anapomaliza elimu yake aweze kukabiliana na changamoto binafsi, mazingira yanayomzunguka, na kuweza kushindana katika soko la ajira kimataifa.

Naye kiongozi wa wataalamu walioandaa andiko la rasimu ya mapendekezo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TSC, Wakili Richard Odongo amesema kuwa timu hiyo ilipitia Sheria na Kanuni zote zinazomhusu mwalimu na kutoa mapendekezo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuongeza tija katika kumhudumia mwalimu.

Timu hiyo ilihusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama akifungua kikao kazi kikao kazi cha kupitia andiko la rasimu ya mapendekezo ya kuhuisha sheria na kanuni zote zinazohusu mzunguko wa mwalimu kinachofanyika Machi 1 – 3, 2023 mjini Morogoro.

Washiriki wa Kikao Kazi cha kupitia rasimu ya mapitio ya Sheria na Kanuni zote zinazumhusu mwalimu wakiendelea na kikao.



No comments