NYUMBA YA NYERERE NA SAMORA ZILIVYOGEUKA KIVUTIO ENEO LA MASONYA TUNDURU
Na
Albano Midelo
ENEO
la Masonya lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma lina
utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa kimataifa.
Eneo
hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa malikale
ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia na kuishi Marais
Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro Machel wa Msumbiji kuanzia
1966 wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mkurugenzi
wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema viongozi hao pia
wakiwa katika nyumba hiyo walitumia kibanda maalum kilichopo jirani ya nyumba
hiyo kama chumba cha mawasiliano na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi
kusini mwa Afrika.
Masonya
ni eneo la hifadhi ya Makumbusho ya kihistoria ya watu wa Msumbij,ambalo
limesheni utajiri mkubwa wa historia ya Tanzania na namna Tanzania
ilivyoshiriki katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika.
Jambo
la kufurahisha zaidi eneo hili lina nyumba iliyotumiwa na Rais wa zamani wa
Msumbiji hayati Samora Machel kuanzia mwaka 1966 hadi nchi hiyo ilipopata uhuru
mwaka 1975.
Mkurugenzi
wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anasema mwaka 1966 Tanzania iliwapokea wapigania uhuru wa Msumbiji na kuwakabidhi
eneo la Masonya lililopo kilometa nane toka Tunduru mjini.
Hata
hivyo anasema eneo hili limebaki kama eneo la makumbusho ambapo ametaja urithi
unaopatikana katika eneo hilo kuwa ni nyumba mbili za viongozi wa kitaifa
hayati Samora Machel Rais wa kwanza wa Msumbiji na Nyumba aliyokuwa anafikia
baba wa Taifa hayati Julius Nyerere.
Nyamusya
ameutaja urithi mwingine kuwa ni jengo moja la mawasiliano alilokuwa anatumia
Rais Samora Machael,ukumbi wa semina aliokuwa anatumia Samora Machel kutoa
mafunzo mbalimbali na majengo 11 ambayo kwa sasa ni madarasa ya wanafunzi wa
sekondari ya wasichana Masonya.
“Maeneo
mengine ya urithi ni mahandaki yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Msumbiji,eneo
la bendera ya FRELIMO na eneo la mnara ulipofanyika mkutano wa wanawake wa
Msumbiji tarehe 17/3/1973 ‘’, anasema Mkurugenzi wa Makumbusho ya Majimaji.
Kulingana
na Nyamusya mwaka 1975 baada ya nchi ya Msumbiji kupata uhuru wapigania uhuru
hao walirudi katika nchi kwao na kuanzia mwaka
1990 Halmashauri ya Tunduru iliamua kuanzisha shule ya sekondari ya
wasichana Masonya ambayo hadi kufikia mwaka 2014 inachukua wanafunzi wa kidato
cha kwanza hadi cha sita.
Tito
Mboma ni Mwalimu wa sekondari ya wasichana Masonya na Mtaalam wa Makumbusho ya
Masonya,amesema Rais wa sasa wa Msumbiji Philip Nyusi amesoma shule ya msingi
FRELIMO katika eneo la Masonya na kwamba alifika hapo mwaka 1970 akiwa na umri
wa miaka nane.
Serikali
hivi sasa inalitumia eneo la malikale la Masonya kwa shughuli za kielimu ambapo
katika eneo hilo imejenga shule ya sekondari ya Masonya kuanzia kidato cha
kwanza hadi cha sita.
Historia
inaonesha kuwa kabla ya mwaka 1966,eneo la malikale la Masonya lilikuwa ni
msitu ambapo katika mwaka huo ndipo serikali iliwapokea watu kutoka nchini
Msumbiji na kuwakabidhi eneo hilo katika
kipindi chote cha kupigania uhuru nchini Msumbiji toka katika utawala wa Mreno.
Erick
Soko ni Afisa Elimu Msaidizi Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anasema tangu
tangu wakabidhiwe eneo hilo la Masonya watu wa Msumbiji mwaka 1966,wamewahi
kutembelea na kuishi kadhaa viongozi mashuhuri akiwemo Hayati Samora Machel
ambaye alifika mara kadhaa wakati wa harakati za kupigania uhuru.
Soko
anabainisha zaidi kuwa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 1966 hadi wanawake
toka nchini Msumbiji wameishi katika eneo la Masonya na kwamba Umoja wa
Wanawake wa Msumbiji uliojulikana kwa OMM ulianzia Masonya mwaka 1973.
Mwaka
1975 baada ya uhuru wa Msumbiji
kutangazwa ndipo kambi ya Masonya ilivunjwa na wanamsumbiji walirejea katika
nchi yao,tangu mwaka 1975 hadi mwaka 1989 eneo hili lilibaki bila matumizi hadi
mwaka 1990 ilipoanzishwa sekondari ya wasichana Masonya.
Imeadikwa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma.
Post a Comment