REJA-ASISITIZA KUTUNZWA VIZURI NYARAKA NA KUMBUKUMBU ZA CCM
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM),kimesema kitaendelea kutunza,kuhifadhi na kudhibiti zisiharibiwe kumbukumbu na nyaraka zake za kihistoria ili ziwanufaishe vizazi vya sasa na vijavyo.
Hayo ameyasema Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Taifa
Salum Khatib Reja,wakati akitembelea na kukagua maeneo ya historia ya CCM yaliopo maeneo ya Unguja ambapo alisema lengo la ziara hiyo ni kuyajua na kuyatambua maeneo yote ya historia ya chama.
Alisema kumbukumbu hizo zimebeba historia halisi ya CCM inayotakiwa kuenziwa na kulindwa kikamilifu.
Katibu huyo alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la 2022 ibara ya 107(2)(f) inayotoa maelekezo kwa Idara ya itikadi na uenezi ina wajibu wa kutekeleza jukumu la kutunza kumbukumbu hizo za chama.
"Idara ya Itikadi na Uenezi ndio imepewa jukumu na chama la kuhifadhi na kuendeleza historia ya chama hivyo tuhakikishe tunatekeleza majukumu haya tuliopewa,"alisema
Mbali na hilo,Katibu huyo pia aliwataka watendaji wa CCM kuanzia ngazi ya Mkoa na Wilaya kuanza kutengeneza mifumo mizuri ya kutunza kumbukumbu za chama tangia kuzaliwa kwake.
Pamoja na hayo alisema Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ni sehemu ya mambo makuu yanayojenga historia ya CCM, hivyo kuna umuhimu wa jamii kujifunza historia hiyo.
Aliziagiza ofisi ya CCM kuanzia mkoa hadi wilaya kuweka historia ya kuonyesha idadi ya makatibu wa ngazi hizo waliongoza tangu kipindi cha mwaka 1977.
"Lazima tuwe na ubao ofisi za chama ambao utaonyesha katibu wa kwanza wa CCM alikuwa nani alikuwa katibu kuanzia lini mpaka lini,"alisema
Katibu huyo alisema kuna baadhi ya kielelezo cha historia bado hakijahifadhiwa kwenye kumbukumbu ikiwemo eneo la Mbuzini ambalo lina historia kubwa kwa chama.
"Kwenye kumbukumbu eneo la Kilombero lipo lakini hili eneo la Mbuzini bado hatujaweka kumbukumbu licha ya kuwa lina historia kubwa kutokana na kuwa ASP ilinunua eneo hili kwa ajili ya kuzikana wanachama waliobaguliwa enzi za ukoloni.,"alisema
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis alisema Idara yake itahakikisha inahifadhi na kuzitunza vielezo vyote vya kihistoria vya chama.
Alisema idara hiyo ina mpango wa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wake juu ya masuala mbalimbali ya historia ili kuwajenga kisaikolojia waendelee kuwa wazalendo.
Katibu huyo wa sekretarieti Taifa Roja, alitembelea maeneo mbalimbali ya CCM yakiwemo Ofisi ya CCM Wilaya ya Mjini iliyokuwa Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa ASPYL pia lilitumika kuwapokea wapigania uhuru wa Chama cha frelimo na katika jingo la Chama cha Shiraz Association lilipo Kijangwani.
Nyingine ni taasisi ya nyaraka na kumbukumbu kilimani Zanzibar, kituo cha radio bahari FM,iliyokuwa nyumba ya ASP katika eneo la Muembe Kisonge,iliyokuwa nyumba ya vijana wa chipukizi wa zamani(YASO) pamoja na iliyokuwa nyumba ya chama cha African Association iliyopo kikwajuni.
Maeneo mengine ni iliyokuwa nyumba ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Aman Karume iliyopo Kisima Majongoo Kikwajuni pamoja na nyumba ya Wananchi Forodhani na jingo la ASP lililopo Kijangwani.
Aidha, maeneo mengine yaliyotembelewa ni shamba la CCM lililopo Kilombero,eneo alipozaliwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume,shamba la ASP lililonunuliwa kwa ajili ya kuzika wanachama wake waliotengwa na wakoloni,kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu Aboud Jumbe pamoja na kaburi la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume.
KATIBU wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Taifa Salum Khatib Reja,akiwa na watendaji mbalimbali wa Chama na Jumuiya wakikagua nyumba ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume iliyopo Mwera Unguja.
KATIBU wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Taifa Salum Khatib Reja,pamoja na viongozi wengine na familia wakiomba dua katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Aboud Jumbe.
Post a Comment