SIMBA SC WATUMA SALAMU HOROYA
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar FC kwenye Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC PL) uliopatikana kwenye uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro huenda ikawa si shabaha kubwa ya Simba SC kupata ushindi huo na kupata alama tatu muhimu kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi hiyo ya NBC.
Shabaha ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ni Machi 18, 2023 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Horoya AC ya Guinea kwenye mtanange wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAF CL) ikiwa ni mchezo wa tano wa Kundi C la Michuano hiyo.
Katika mchezo huo muhimu, Simba SC wanapaswa kupata ushindi dhidi ya miamba hiyo ya soka kutoka nchini Guinea. Matokeo pekee yatakayoipeleka Simba SC hatua ya Robo Fainali ni ushindi kutokana na mahesabu ya msimamo wa Kundi lenyewe ambalo linaongozwa na Raja Casablanca wenye alama 12 na tayari wamefuzu Robo Fainali
Simba SC wapo nafasi ya pili wakiwa na alama sita, huku Horoya AC wakiwa na alama nne na Vipers SC ya Uganda inaburuza mkia na alama moja pekee na tayari wameaga mashindano. Simba SC wanapaswa kupata ushindi dhidi ya Horoya ili kufika alama tisa ambazo zitakuwa hazifikiwi na timu ya Horoya AC na Vipers SC hata wakikutana kwenye mchezo wao wa mwisho.
Endapo Simba SC itajihakikishia ushindi na kukusanya jumla ya alama tisa katika Kundi hilo watakuwa wamefuzu moja kwa moja hatua ya Robo Fainali ya Michuano hiyo, na watakamilisha ratiba kwa kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Raja Casablanca nchini Morocco huku Horoya wakiwa nyumbani watakamilisha ratiba dhidi ya Vipers SC.
Post a Comment