TANESCO SINGIDA MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA WATEKELEZA MIRADI YA SHILINGI BILIONI 4.8
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ambapo alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida kwa kutekeleza miradi 113 ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.8.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amesema miradi
113 ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.8 imetekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida katika kipindi
cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutumia fedha za ndani.
Serukamba ameyasema hayo jana Machi 18, 2023, mjini hapa, wakati akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dk.Samia.
“Hali ya upatikanaji umeme ni ya kuridhisha kwa wilaya zote, hadi sasa jumla ya vijiji 318 sawa na asilimia 72.11 kati ya 441 vilivyo sajiliwa vimeunganishwa umeme wa gridi ya taifa,” alisema Serukamba.
Alifafanua kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa,
linaloongozwa na Meneja wake, Mhandisi Florence Mwakasege, linasimamia miradi mikubwa
minne ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), kwenye vijiji 123 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 73.
“Mkoa uliwaunganishia wateja wapya 19,223
wanaojumuisha shule 287, zahanati 75, visima vya maji 23, viwanda vidogo 76,
migodi mitano ya madini ya dhahabu, misikiti 43, makanisa 60, mahakama mbili na
vituo 102 vya kibiashara,” alisema Serukamba.
Alibainisha kuwa wapo wakandarasi katika vijiji 123
kukiwa na matarajio ya kuwasha vijiji 13 ifikapo Machi 30, 2023 na vingine vilivyo
baki ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Post a Comment