Header Ads

test

MFUMO WA STAKABADHI GHALANI WAWAINGIZIA WAKULIMA RUVUMA ZAIDI YA BILIONI 87

WAKULIMA mkoani Ruvuma wameweza kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 87 baada ya kuuza mazao ya ufuta,soya,mbaazi,korosho na kahawa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika kipindi cha mwaka 2022/2023.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katika hotuba yake iliyosomwa na Mwakilishi wake Mhe.Kapenjama Ndile kwenye jukwaa la maendeleo ya ushirika Mkoa wa Ruvuma lililofanyika katika ukumbi wa Chandamali mjini Songea.

Kanali Thomas amesema kati ya fedha hizo wakulima waliuza ufuta tani 7,970 zilizowaingizia shilingi bilioni 5.97 na mbaazi tani 6,647 zilizowaingizia shilingi bilioni 5.21.

Amebainisha zaidi kuwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima mkoani Ruvuma,waliuza korosho tani 15,315 zilizowaingizia shilingi bilioni 23.9 na kwamba waliuza kahawa tani 4,856 zilizowaingizia wakulima shilingi bilioni 31.61.

“Natoa wito kwa Halmashauri zote na viongozi katika ngazi zote tuwe na mpango kabambe wa kusimamia mfumo wa stakabadhi ya ghala na wakulima kujiunga na kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi za vyama vya ushirika’’,alisisitiza Kanali Thomas.

Amewatahadharisha wadau wa ushirika kutowaruhusu wanaotaka kupindisha sheria kwa sababu wataua ushirika na kwamba wasiruhusiwe wafanyabiashara au mtu yeyote anayetaka kukwamisha mfumo wa stakabadhi ghalani.

Amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 itahakikisha dhana ya ushirika wa hiari inajengwa na kusimamiwa na sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha wanaushirika hivyo kuchangia ustawi wa
ushirika na Taifa kwa ujumla.

Awali Stella Msengi akisoma risala ya wanaushirika na wadau wa maendeleo ya ushirika katika Jukwaa la Ushirika wa Mkoa wa Ruvuma, amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufanyia kazi
changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili jamii kupitia vyama vya
ushirika.

Amesema Mkoa wa Ruvuma hadi sasa una jumla ya vyama vya ushirika 293 kati ya hivyo vyama vya ushirika vya akiba na mikopo ni 62,vyama vya ushirika wa masoko ya mazao 222 vyama vikuu vya ushirika vitatu na vyama vya ushirika vinginevyo sita.

Risala hiyo imeyataja baadhi ya mafanikio ya vyama vya ushirika katika Mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuratibu upatikanaji wa pembejeo,kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao na bidhaa,kusimamia masoko ya mazao na bidhaa na kusimamia matumizi ya vipimo sahihi vya mauzo ya mazao
ya wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Ruvuma Justine Welo amesema ushirika ni Taasisi ambayo inapigwa vita na watu wanaotaka kuwanyonya wakulima kwa kuwa ushirika unahusika na mazao ya kimkakati kama kahawa na korosho.

Amesisitiza kuwa katika kipindi cha mavuno kumekuwa na vita ya kugombea mazao hayo hivyo ametoa rai kwa serikali kuweka sheria ya Ushirika kusimamia mazao ya kimkakati.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya Jukwaa la Ushirika ni Ushirika kwa maendeleo endelevu.wadau wa ushirika kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Ruvuma (JUMRA) lililofanyika kwenye ukumbi wa Chandamali Mahenge mjini Songea.


Mkurugenzi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Juma Mokiri akizungumza kwenye Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Ruvuma.Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja akizungumza kwenye Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Ruvuma.Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Kapenjama Ndile akifungua Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Ruvuma lililofanyika kwenye ukumbi wa Chandamali mjini Songea.

 

No comments