MIILI MINGINE 11 YAFUKULIWA....IDADI WALIOKUFA KANISA TATA LA MACKENZIE NI 145
Miili kumi na moja zaidi imefukuliwa leo Jumatano katika msitu wa Shakahola pwani ya Kenya na kufanya idadi ya watu waliofariki wakifunga kula chakula kwa maelekezo ya mhubiri wao Paul Mackenzie kufikia 145.
Kufikia sasa watu zaidi ya mia tano bado hawajulikani waliko polisi wakiendelea na zoezi la ufukuaji zaidi wakati huu pia watu wengine wawili wakiripotiwa kuokolewa kutoka katika msitu huo.
Taarifa mpya zinaonyesha kuwa baadhi ya waathirika wa mauaji ya Shakahola walipatikana na viungo vya mwili vilivyopotea.
Uvunaji wa viungo Inadaiwa kuwa waathirika wanaoaminika kuwa washirika wa Kanisa la Good News International la pasta Paul Mackenzie, huenda viungo vyao vilivunwa kabla ya kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini, Inspekta Mkuu Martin Munene alisema kwamba upasuaji uliofanywa na mpasuaji mkuu wa serikali Johansen Oduor ulithibitisha kuwa baadhi ya miili iliyofukuliwa haikuwa na viungo.
"Inaaminika kwamba biashara ya viungo vya mwili wa binadamu ina mtandao unaohusishwa na watu kadhaa. Inashukiwa kwamba miili zaidi inaweza bado iko kuzikwa katika ardhi kubwa inayofunika ekari zaidi ya 1,000," Munene alisema, kama ilivyonukuliwa na Nation.
Munene alisema wanajaribu kuona jinsi Mackenzie atakavohusishwa na biashara ya ulanguzi wa viungo vya binadamu. Afisa huyo aliongeza kwamba Mackenzie na pasta Ezekiel Odero wanashukiwa kuwa na uhusiano wa karibu.
Post a Comment