BoT YATOA TAARIFA KUHUSU KUHAMISHA MALI NA MADENI YAO MICROFINANCE BANK PLC KWENDA NMB BANK PLC
Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria cha 56(1)(g)(i) na (iii) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, mnamo tarehe 12 Disemba 2022 Benki Kuu ya Tanzania iliiweka chini ya usimamizi wake Yetu Microfinance Bank Plc kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili ya mtaji na ukwasi. Shughuli za kawaida za biashara za Yetu Microfinance Bank zilisimamishwa kuiwezesha Benki Kuu kutathmini hatua stahiki za kuchukua.
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuujulisha umma kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 59(4) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 mchakato wa kupata suluhisho la Yetu Microfinance Bank Plc umekamilika, na uhamishaji wa mali na madeni kwenda benki nyingine ndio hatua stahiki iliyofikiwa. Hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 58(2)(h) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imehamisha mali na madeni ya Yetu Microfinance Bank Plc kwenda NMB Bank Plc kuanzia tarehe 24 Mei 2023.
Wenye amana na wadai wengine wa Yetu Microfinance Bank Plc watapewa taarifa ya namna na siku watakayoanza kupata huduma za kibenki kupitia benki ya NMB. Wakati huo huo, wateja wote wenye mikopo wanatakiwa kuendelea kulipa marejesho yao kwa mujibu ya mikataba yao ya mikopo.
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya kibenki.
Post a Comment