MADEREVA NA MAKONDAKTA MKOANI TANGA WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO.
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KAMANDA
wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Willy Mwamasika amesema madereva
wana mchango mkubwa katika kuimarisha na kukuza uchumi hivyo wana wajibu
mkubwa wa kufanya kazi zao kwa weledi ili kuepusha madhara kwa
wananchi.
Mwamasika
ameyasema hayo wakati akiongea na madereva pamoja na makondakta katika
stendi kubwa ya mabasi yaendayo Mikoani iliyopo Kange jijini Tanga kwa
lengo la kuwakumbusha wajibu wao wakiwa kazini.
"Kila
mtu ana nafasi yake katika uchangiaji wa uchumi, kwahiyo na ninyi hii
kazi mnayoifanya mna mchango wenu katika ukuaji wa uchumi wa Tanga,
ilimradi tu katika utekelezaji wenu mhakikishe hamvunji sheria,
kwasababu mnabeba abiria kuwawahisha katika majukumu yao ya kuchangia
uchumi,
"Hivyo basi mna
wajibu wa kuchukua tahadhari zote mnapokuwa barabarani ili kuhakikisha
hamleti madhara kwa abiria wenu, madereva wana wajibu wa kuhakikisha
wanaendesha kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa
Sheria ya Usafirishaji" amesema.
Aidha
Mwamasika amewataka madereva hao kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka
kusumbuana na askari wa barabarani kwani itasaidia kila mmoja kuwa na
uhuru anapokuwa katika eneo lake la kazi.
Mwamasika
pia amepiga marufuku kwa maajenti wanaotafuta abiria kuwafanyia
usumbufu kwa kuwavuta na kusababisha kero kwa abiria hao, ikiwa ni
pamoja na vibaka wanaokwenda stendi kwa ajili ya kutekeleza wajibu wao
wa kuibia watu.
"Ni
matumaini yangu mmenielewa na mtatekeleza majukumu yenu ipasavyo, nite
onyo kwa wale wenzetu ambao wanakuja stendi kwa ajili ya kufanya wizi wa
kuibia wasafiri, stendi yetu ni nzuri na haina dosari hivyo watu hawa
ni marufuku kuingia hapa, hawana nafasi kwqni hawa ndio wanaotuharibia"
amesema.
"Na ninyi
mnaofanya kazi zenu za kutafuta abiria hapa mtoe taarifa kuwafichua hawa
vibaka ili tuwaondoe watuachie stendi yetu, nina imagine mtafanya hivyo
ili tunapokutana barabarani tuwe tunapungiana na sio kufuatana mwisho
wa siku tunachukiana" ameongeza.
Hata
hivyo Mwamasika amewaasa madereva wanaendesha mwendo wa kasi kufuata
maelekezo ya serikali kwa kutembea mwendo wa kawaida uliopangwa kwakuwa
atakayekiuka mbali na adhabu lakini pia ipo adhabu kubwa ya kufutiwa
leseni aliyonayo ili akaanze upya kuipata.
"Nadhani
mmenielewa madereva, tembeeni mwendo wa serikali, sasa hivi dunia ni
kama kijiji, usije ukasema hatukuoni huko barabarani, ulipo na sisi
tupo, kwa atakayekiuka agizo hilo atapigwa faini na atakapoendelea
atalazimika kufungiwa leseni, na atakapofungiwa atalazimika kuanza upya
kuomba, lakini pia tutakuangalia kama utakuwa na vigezo, usipotimiza
uachane na udereva unde ukatafute kazi za kufanya" amesema.
Vilevile
ametoa wito kwa madereva wote wa mabasi makubwa na daladala kuanzia
wenye madaraja class C na E, kwamba zoezi la uhakiki wa leseni hizo wa
hiyari bado linaendelea, na baada ya muda ukifika serikali itaanza msako
wa kukamata madereva ambao hawajahakiki leseni zao.
"Sasa
hivi njoo na leseni yako tukuhakiki kama ni halali tutakupa barua ya
kutembea nayo kwamba wewe umehakikiwa na upo kihalali, lakini suala la
upatikanaji wa leseni ni lazima ukasome, nendeni kwenye vyuo
vinavyotambulika kisheria, baada ya hapo ulete barua ya maombi na
utapatiwa keseni kulingana na madaraja ya chuo ulichosomea" amebainisha.
Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Willy Mwamasika akiongea na
madereva pamoja na makondakta katika stendi kubwa ya mabasi yaendayo
Mikoani iliyopo Kange jijini Tanga.
Post a Comment