Header Ads

test

WAKULIMA WA UFUTA NAMTUMBO KICHEKO,WAFURAHIA BEI NA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Na Muhidin Amri, Namtumbo


WAKULIMA wa zao la ufuta wilayani Namtumbo, wamekubali kuuza zao hilo kwa bei ya Sh.3,701 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika kijiji cha Limamu huku wakulima wakiipongeza Serikali kwa kusimamia soko la zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Katika mnada huo jumla ya makampuni 17 yamejitokeza kununua ufuta,ambapo kilo 471,223 zilizokusanywa na Chama cha msingi cha Ushirika(Amcos) Limamu kutoka kwa wakulima zimeuzwa kupitia mfumo huo.

Wakulima wamesema,mfumo wa stakabadhi ghalani una manufaa makubwa kwao kwa sababu unawasaidia kupata soko la uhakika na bei nzuri tofauti na soko huria ambalo wafanyabiashara wanatumia nafasi hiyo kuwanyonya.

Moses Mapunda amesema,mfumo wa stakabadhi ghalani una faida kubwa kwa mkulima na kama ungeanzishwa muda mrefu wakulima wengi wangeondokana na tatizo la umaskini kwenye familia zao.

Amesema kuwa,mfumo huo ni rafiki kwani tangu ulipoanzishwa umesaidia sana kuhamasisha wakulima wengi kuongeza uzalishaji wa mzao mashambani kwa sababu wana uhakika wa kupata fedha nyingi kupitia shughuli zao za kilimo.

Adam Mapunda,ameiomba serikali kuendelea kuimarisha ununuzi wa mazao kupitia mfumo huo ili kutowapa nafasi wafanyabiashara kununua mazao kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi ya uzalishaji.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaotaka kununua zao hilo nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani.

Malenya,ameliagiza jeshi la Polisi wilayani humo kushirikiana na wenyeviti,watendaji wa vijiji na kata kuwakamata na kuwachukulia hatua kali madalali wa ufuta wanaojifanya wafanyabiashara wanaopita vijijini ili kuwarubuni wakulima wauze ufuta kwa bei ndogo.

Alisema,lengo la serikali kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ni kuwasaidia wakulima kuwa na soko la uhakika,kupata bei nzuri na kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za uzalishaji wa mazao.

Mkuu huyo wa wilaya,amewataka wakulima wilayani humo kukataa kuuza mazao kwa bei ndogo na nje ya mfumo huo,badala yake watumie vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS)vyenje dhamana ya kukusanya mazao na kuuza kupitia minada mbalimbali katika maeneo yao.

Amewaasa wakulima kubadilika na kutumia fedha wanazopata kubadili maisha yao kwa kujenga nyumba bora na kusomesha watoto wao,badala ya kutumia katika mambo ya anasa ikiwemo unywaji wa pombe.

Aidha amesema,kuanzia msimu mpya wa kilimo 2023/2024 mbolea zitapelekwa kila kijiji ili kurahisisha upatikanaji wake na kuwaondolea usumbufu wakulima wa kufuata mbolea hizo makao makuu ya wilaya.

Awali Afisa shughuli wa Chama kikuu cha Ushirika Sonamcu Zamakanal Komba amesema,mfumo wa uendeshaji wa minada mwaka huu utafanyika vijijini badala ya mjini kama ilivyozoeleka ili kutoa fursa kwa wakulima kutambua na kufahamu namna ya uendeshaji wa minada na bei ya mazao yao.

Amesema,katika msimu wa kilimo 2022/2023 jumla ya minada 12 ya ufuta ilifanyika ambapo wastani wa bei ya juu ilikuwa Sh. 2,900 na bei ya chini ilikuwa Sh.2,800.



No comments